Mvua kubwa yauwa watu 2 na kujeruhi 40 katika mji wa Sabha, Libya
(last modified Mon, 16 Sep 2024 02:33:02 GMT )
Sep 16, 2024 02:33 UTC
  • Mvua kubwa yauwa watu 2 na kujeruhi 40 katika mji wa Sabha, Libya

Takriban watu wawili wamepoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika mji wa Sabha, kusini mwa Libya jana Jumapili.

Belhaj Ali, Meya wa mji wa Sabha amesema kuwa mafuriko yamepelekea nyumba nyingi kuzama. Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Sabha kwa upande wake limewataka wananchi wote kufuata maelekezo ya usalama ili kuepusha matukio zaidi ya maafa.  

Mafuriko yaukumba mji wa Sebha, Libya 

Kituo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha Libya kilitahadharisha juzi Jumamosi  kuhusu mvua kubwa itakayonyesha na kuambatana na mingurumo ya radi kusini mwa nchi ambayo inaweza kusababisha mito kujaa maji na kusababisha mafuriko.

Inafaa kuashiria hapa kuwa Libya kwa sasa inaongozwa na serikali mbili hasimu. Serikali ya kwanza ni ile ya umoja wa kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa (GNU) inayoongozwa na Abdul Hamid Dbeibeh yenye makao yake mjini Tripoli ikidhibiti eneo la magharibi mwa nchi hiyo, na serikali ya pili inaongozwa na Osama Hammad, iliyoteuliwa na bunge, ambayo inafanya kazi zake katika mji wa Benghazi ikisimamia  eneo la mashariki na sehemu za kusini mwa Libya.