China kusaidia ujenzi wa kiwanda cha kwanza Afrika cha chanjo ya kipindupindu nchini Zambia
Oct 09, 2024 02:26 UTC
Zambia imetia saini Hati ya Makubaliano (MOU) na China ya ujenzi wa kiwanda cha kwanza cha utengenezaji chanjo ya kipindupindu nchini humo na barani Afrika pia.
Awamu ya kwanza ya mradi huo itagharimu dola milioni 37, wakati dozi zipatazo milioni tatu zikitarajiwa kutengenezwa kwa njia ya ubia kati ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Zambia (IDC) na Shirika la Kimataifa la Jijia la Teknolojia ya Tiba (Jijia International Medical Technology Corporation).
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano hayo katika Ikulu ya mji mkuu Lusaka, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amesema, maendeleo hayo ni hatua muhimu katika azma ya nchi hiyo ya kutokomeza ugonjwa huo ambao unaathiri uzalishaji kutokana na kuathiri wananchi wake.
Hichilema amesema, kipindupindu kingali ni tishio kubwa kwa Upande wa Kusini mwa Dunia, kwa kuathiri watu bilioni 1.3 ulimwenguni kote na kusababisha maambukizi milioni 2.86 na karibu vifo 95,000 kila mwaka.
Aidha, Rais wa Zambia amesifu ushirikiano uliopo katia ya nchi yake na China na kusema: "tunamshukuru sana Rais Xi Jinping na watu wa China kwa ushirikiano wao katika kufanikisha dira hii".
Ujenzi wa kiwanda hicho cha chanjo ya kipindupindu unaashiria hatua muhimu iliyopigwa katika mkakati wa afya ya umma nchini Zambia na kuimarisha nafasi yake katika kuongoza kampeni ya kimataifa ya kuutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Mradi huo unatazamiwa kutoa fursa za ajira, msukumo kwa uchumi wa ndani, na kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za ugonjwa wa kipindupindu barani Afrika.../