Nandi-Ndaitwah atangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi na kuwa rais wa kwanza mwanamke Namibia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119688-nandi_ndaitwah_atangazwa_rasmi_mshindi_wa_uchaguzi_na_kuwa_rais_wa_kwanza_mwanamke_namibia
Namibia imepata rais wake wa kwanza mwanamke baada ya mgombea wa chama tawala cha SWAPO na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Bi Netumbo Nandi-Ndaitwah mwenye umri wa miaka 72, kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika wiki iliyopita.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Dec 04, 2024 03:09 UTC
  • Nandi-Ndaitwah atangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi na kuwa rais wa kwanza mwanamke Namibia

Namibia imepata rais wake wa kwanza mwanamke baada ya mgombea wa chama tawala cha SWAPO na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Bi Netumbo Nandi-Ndaitwah mwenye umri wa miaka 72, kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa jana na Tume ya Uchaguzi ya Namibia ECN, Nandi-Ndaitwah amepata 57.31% ya kura, akiwashinda wagombea wengine 14 na kuvuka kizingiti cha 50% ili kuepusha uchaguzi huo kuingia duru ya pili.
 
"Kwa mujibu wa Kifungu cha 109 cha Sheria ya Uchaguzi...mimi, Elsie Nhikembua, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Namibia, namtangaza Mheshimiwa Netumbo Nandi-Ndaitwah wa chama cha SWAPO kama mshindi na rais mteule wa uchaguzi wa urais wa 2024," alitamka Nghikembua wakati akitangaza matokeo ya uchaguzi huo katika mji mkuu, Windhoek.
 
Nandi-Ndaitwah atakuwa rais wa tano wa Namibia na kiongozi wa nne mwanamke barani Afrika baada ya Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia aliyeongoza nchi hiyo kati ya mwaka 2006 na 2018, Joyce Banda wa Malawi kutoka 2012 hadi 2014 na Samia Suluhu Hassan wa Tanzania aliyeko madarakani hivi sasa.
 
Rais mteule wa Namibia, hapo awali alikuwa naibuu mkuu wa chama cha SWAPO chini ya uongozi wa Rais Hage Geingob, aliyeaga dunia Februari 2024 na kuwa makamu wa Rais kwa Rais anayemaliza muda wake Nangolo Mbumba, ambaye alishika jukumu la kuongoza kipindi cha mpito baada ya kifo cha Geingob.
 
Matokeo hayo ya uchaguzi yametangazwa katika hali ambayo, mgombea mkuu wa urais wa upinzani Panduleni Itula, alitangaza siku ya Jumamosi kuwa chama chake hakitatambua matokeo ya uchaguzi huo uliokuwa umekumbwa na utata wa kuongezewa muda wa upigaji kura na kutawaliwa na fujo na madai ya uchakachuaji.../