Ukatili wa kijinsia unazidi kuongezeka Kenya, matukio zaidi ya 7,000 yameripotiwa katika mwaka mmoja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120578-ukatili_wa_kijinsia_unazidi_kuongezeka_kenya_matukio_zaidi_ya_7_000_yameripotiwa_katika_mwaka_mmoja
Kenya inakabiliwa na ongezeko la kutisha la ukatili wa kijinsia, baada ya kesi zaidi ya 7,100 kuripotiwa tangu Septemba 2023, ikiwa ni pamoja na mauaji 100 yaliyorekodiwa ya wanawake tangu Agosti mwaka huu. Hayo ni kwa mujibu wa rekodi za serikali.
(last modified 2026-05-19T09:45:50+00:00 )
Dec 25, 2024 03:24 UTC
  • Ukatili wa kijinsia unazidi kuongezeka Kenya, matukio zaidi ya 7,000 yameripotiwa katika mwaka mmoja

Kenya inakabiliwa na ongezeko la kutisha la ukatili wa kijinsia, baada ya kesi zaidi ya 7,100 kuripotiwa tangu Septemba 2023, ikiwa ni pamoja na mauaji 100 yaliyorekodiwa ya wanawake tangu Agosti mwaka huu. Hayo ni kwa mujibu wa rekodi za serikali.

Miongoni mwa manusura wa ukatili huo ni Sarah Wambui, ambaye alifikwa na mkasa wa kushambuliwa kwa kisu na mumewe aliyeishi naye kwa miaka 20.
"Alinidunga kisu mara 38 mnamo Januari 18, 2024, na kuathiri hata figo langu na ini," amesimulia mwanamama huyo ambaye alitoka hospitalini mnamo mwezi Agosti. 
Wambui anasema, sasa anaishi kwa hofu huku aliyemshambulia akisalia huru, akidaiwa kutishia pia maisha yake.
"Kwa sasa, maisha yangu yako hatarini," Wambui amesema na kuongeza kuwa: "mhusika yuko nje, na ameapa kunimaliza."
 
Kukitihiri kwa ukatili wa kijinsia nchini Kenya kumeamsha ghadhabu kitaifa, ambapo wiki mbili zilizopita yalifanyika maandamano makubwa ya wanawake jijini Nairobi, kudai haki na kuitaka serikali pia ichukue hatua. Polisi waliwatawanya waandamanaji kwa gesi ya kutoa machozi na kuwatia mbaroni kadhaa miongoni mwao, jambo lililosababisha ukosoaji mkali kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu.
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani Musalia Mudavadi amekiri kukithiri kwa janga hilo na kueleza kwamba Kaunti ya Nairobi ilirekodi idadi kubwa zaidi ya visa vya ukatili wa kijinsia, huku kaunti za mashambani kama Samburu na Mandera zikiwa na idadi ndogo zaidi.
Mudavadi ameongeza kuwa, uchunguzi wa mauaji mengi kati ya 100 umekamilika, na kesi zake zinaendelea kusikilizwa mahakamani.

Hata hivyo watetezi wa haki za binadamu wameeleza kuwa ukubwa halisi wa tatizo hilo unaweza ukawa wa hali mbaya zaidi.
Njoki Gachanja, mtafiti wa haki za binadamu amesema: "matukio mengi yanapita bila kurekodiwa, hasa katika maeneo ya watu wenye kipato cha chini ambapo umaskini na kanuni za mfumo dume huchochea ukatili".
Kwa mujibu wa Kituo cha Kuhudumia Waathirika wa Ukatili wa Kijinsia, mmoja kati ya wanawake watatu nchini Kenya hufanyiwa ukatili wa kijinsia kabla ya kufikisha miaka 18, na 38% ya wanawake walioolewa wanakabiliwa na ukatili wa kimwili.
 
Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali ya Nairobi imeanzisha kikosi maalumu cha usalama kushughulikia janga hilo na kuhakikisha haki inatendeka. Wanaharakati, hata hivyo, wanataka hatua madhubuti zaidi zichukuliwe kulinda wanawake na wasichana, wakisisitiza kuwa janga hilo haliwezi kupuuzwa tena.../