AU yapongeza mkutano wa viongozi wa Somalia na Ethiopia kufuatia mapatano ya Ankara
(last modified Wed, 15 Jan 2025 07:41:03 GMT )
Jan 15, 2025 07:41 UTC
  • AU yapongeza mkutano wa viongozi wa Somalia na Ethiopia kufuatia mapatano ya Ankara

Umoja wa Afrika umepongeza mkutano wa mwishoni mwa wiki kati ya viongozi wa Somalia na Ethiopia mjini Addis Ababa Ethiopia ambao ulifanyika kufuatia Azimio la Ankara.

Mohamed al Amin Souef Mkuu wa Kikosi cha Usaidizi na Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM) ameyataja mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia kuwa hatua muhimu. Amesema, mkutano wa viongozi wa Ethiopia na  Somalia unathibitisha tena ahadi endelevu zilizofikiwa kati ya nchi mbili. 

Rais wa Somalia katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ethiopia mjini Addis Ababa 

Mohamed al Amin Souef pia ni Mwakilishi Maalumu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa ajili ya Somalia.

Azimio la Ankara lilifikiwa mwezi Disemba mwaka jana wakati wa mazungumzo kati ya Ahmed na Mohamud yaliyofanyika Ankara mwenyeji akiwa Rais Recep Tayyip Erdogan  wa Uturuki.

Rais wa Somalia na Waziri Mkuu wa Ethiopia walitangaza katika kikao chao huko Addis Ababa kuwa nchi mbili hizo zimerejesha na kuanza kuimarisha uhusiano kati ya pande mbili kupitia uwakilishi kamili wa kidiplomasia katika miji mikuu yao baada ya kumaliza mzozo uliodumu kwa mwaka mmoja kati ya nchi hizo.