AU yamtaka Trump atazame upya uamuzi wake wa kuiondoa Marekani katika shirika la WHO
Umoja wa Afrika (AU) jana Jumatano ulimtolea wito Rais mpya wa Marekani, Donald Trump, kufikria tena uamuzi wake wa kuiondoa Washington katika Shirika la Afya Duniani (WHO).
Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema katika taarifa aliyoitoa jana kuwa Marekani ilikuwa na umuhimu katika Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kipindi cha zaidi ya miongo saba kama nchi mwanachama wa shirika hilo.
Baada ya kushika hatamu za uongozi, siku ya Jumatatu, Rais Donald Trump wa Marekani alisaini dikrii inayorasimisha kujiondoa nchi hiyo ndani ya WHO.
Dikrii hiyo ya Trump imetaja sababu kadhaa zilizompelekea kuiondoa Marekani katika Shirika la Afya Duniani ambazo alisema ni pamoja na usimamizi mbaya wa WHO kwa janga la Corona, kushindwa kusimamia vyema migogoro mingine ya afya duniani na kushindwa shirika hilo kufanya mageuzi ya haraka yanaohitajika.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ameongeza kuwa, dunia hivi sasa inalitegemea sana Shirika la Afya Duniani (WHO) kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha usalama wa afya ya umma duniani kote.
WHO iliasisiwa Aprili 7 mwaka 1948. Shirika hilo lina nchi wanachama 194 na linafanya kazi katika maeneo zaidi ya 150 katika mabara sita duniani na linawajibika kwa afya ya umma duniani.