Mashambulio ya siku tatu mtawalia ya RSF yaua watu 450 Darfur, magharibi mwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125150-mashambulio_ya_siku_tatu_mtawalia_ya_rsf_yaua_watu_450_darfur_magharibi_mwa_sudan
Harakati ya Jeshi la Ukombozi wa Sudan, inayoongozwa na Minni Arko Minnawi (SLA-Minnawi), gavana wa jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo, imetangaza kuwa watu 450 wameuawa kutokana na mashambulizi ya siku ya tatu mtawalia yaliyofanywa na wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) katika mji wa El Fasher, makao makuu ya eneo hilo, na kwenye kambi za wakimbizi.
(last modified 2026-09-15T11:41:35+00:00 )
Apr 14, 2025 02:41 UTC
  • Mashambulio ya siku tatu mtawalia ya RSF yaua watu 450 Darfur, magharibi mwa Sudan

Harakati ya Jeshi la Ukombozi wa Sudan, inayoongozwa na Minni Arko Minnawi (SLA-Minnawi), gavana wa jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo, imetangaza kuwa watu 450 wameuawa kutokana na mashambulizi ya siku ya tatu mtawalia yaliyofanywa na wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) katika mji wa El Fasher, makao makuu ya eneo hilo, na kwenye kambi za wakimbizi.

SLA imesisitiza kuwa, Jeshi linpaswa lichukue hatua za haraka kuokoa watu wapatao milioni moja na laki tano, ambao ni wakazi wa mji wa El Fasher.
 
Wakati huo huo, serikali ya eneo la Darfur, imeashiria idadi ya watu 320 waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio la RSF kwenye kambi ya Zamzam huko El Fasher na kutangaza: "kinachotokea huko Darfur ni mauaji ya kimbari na jamii ya kimataifa imenyamazia kimya suala hili. Kwa hiyo, kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha mzingiro uliowekewa mji wa El Fasher".
 
Kuhusiana na suala hilo, Gavana wa Darfur  Minni Arko Minnawi amesema watu wapatao 450 wameuawa katika mashambulizi ya siku mfululizo yaliyofanywa na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka katika mji wa  El Fasher na kambi za Zamzam na Abu Shouk.
 
Minnawi ameongezea kwa kusema, "usaidizi wa jeshi la anga kwa vikosi vyetu huko El Fasher umesitishwa".
 
Katika upande mwingine, Muhammad Issa Aliyu, Naibu Gavana wa Darfur, naye pia amesema: "Vikosi vya RSF vinashambulia kinyama raia katika kambi ya Zamzam".
 

Pande mbili za Jeshi la Sudan, SAF na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, RSF zimekuwa zikipigana vita tangu Aprili 2023 ambavyo vimeua zaidi ya watu 20,000 na kuwafanya wengine milioni 14 walazimike kuyahama makazi yao.

Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Hata hivyo utafiti wa wasomi wa Marekani unakadiria idadi ya vifo kuwa ni karibu 130,000.

Jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa zimetoa wito wa kusitishwa vita hivyo, zikitahadharisha kuhusu janga la kibinadamu linalokaribia kuikumba Sudan huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na hatari ya baa la njaa na vifo kutokana na uhaba wa chakula. Mzozo huo umeenea hadi kwenye majimbo 13 kati ya 18 ya Sudan.../