Misri yakosoa wito wa Trump wa kutaka meli za US kupita mfereji wa Suez bila malipo
Wito wa hivi karibuni wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kutaka meli za nchi hiyo zipitie bila malipo kwenye Mfereji wa Suez umezusha shutuma nyingi nchini Misri, ambapo wataalamu wa masuala ya sheria, viongozi wa kisiasa na wananchi wamekosoa vikali matamshi hayo, wakisema kuwa hayana msingi kisheria, na ni tishio kubwa kwa nidhamu ya kimataifa.
Siku ya Jumamosi, Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii waTruth Social kwamba, meli za kijeshi na za kibiashara za Marekani zinapasa kuruhusiwa kusafiri kupitia Mfereji wa Panama na Suez bila malipo. Alidai kuwa njia hizo mbili za majini"hazingekuwepo" bila Marekani na akasema amemwomba Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio "kushughulikia suala hilo."
"Mapendekezo ya Trump kuhusu njia za kimataifa za majini ni tishio kubwa kwa amani ya kimataifa, usalama na utulivu wa umma," Ayman Salama, profesa wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cairo, ameiambia Xinhua. Salama ameashiria Mkataba wa Constantinople wa 1888, ambao ulianzisha kanuni za kimsingi zinazosimamia shughuli za kimataifa na Mfereji wa Suez, kuhifadhi haki ya nchi zote kufaidika na njia hii ya maji ya kimataifa.
Amesema madai ya Trump "yasiyo na msingi kisheria", na ambayo yanapuuza mamlaka ya mataifa ya pwani juu ya maji na malango bahari yao, ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi nyingine, ukiukaji wa wazi wa kanuni ya jumla ya kutoingilia sheria za kimataifa.
Wakati huo huo, Samaa Soliman, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kigeni, Waarabu, na Afrika ya Baraza la Seneti la Misri, amesisitiza kwamba "Misri pekee ndiyo yenye jukumu la kuuhifadhi na kuulinda Mfereji wa Suez," na mapato yanayotokana na ada za usafirishaji wa mfereji huo ni rasilimali halali inayochangia uchumi wa taifa na kuwahudumia raia wa Misri, na hayataathiriwa kwa kisingizio chochote.
Aidha Muungano wa Vyama vya Misri, unaojumuisha takriban vyama 42 vya kisiasa, umelaani vikali kauli ya Trump, na kueleza kuwa "imepuuza uhalisia wa kihistoria." Mzozo huo umezusha mjibizo mkali katika mitandao ya kijamii ya Misri, hasa kuhusiana na pendekezo la Trump kwamba Marekani inastahili pongezi kwa kuwepo mfereji huo.