UN inahitaji msaada wa dharura wa kuwasaidia wahanga 45,000 wa mafuriko Somalia
(last modified Sat, 03 May 2025 02:19:38 GMT )
May 03, 2025 02:19 UTC
  • UN inahitaji msaada wa dharura wa kuwasaidia wahanga 45,000 wa mafuriko Somalia

Shirika moja la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu limesema kuwa linahitaji msaada wa dharura wa haraka wa kusaidia watu 45,000 walioathiriwa na mafuriko kote nchini Somalia.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), watu wanne, wakiwemo watoto wawili, wamepoteza maisha baada ya kusombwa na maji, huku zaidi ya watu 45,000 wakiwa wameathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua katika mikoa mbalimbali ya Somalia tangu tarehe 15 mwezi uliopita wa Aprili.

OCHA imesema kuwa, Mto Shabelle ulipasua kingo zake siku ya Jumatatu katika wilaya ya Jowhar, na kupelekea zaidi ya watu 6,000 kuyahama makazi yao na maji ya mafuriko kujaa katika takriban hekta 11,000 za ardhi.

Taarifa hiyo iliyotolewa mjini Mogadishu imeongeza kuwa: "OCHA imewasiliana na mashirika mbalimbali ili kupata msaada wowote wa dharura kwa ajili ya watu walioathirika, hasa waliopoteza makazi yao."

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kwamba, mafuriko hayo yametokea wakati mashirika ya kitaifa yasiyo ya kiserikali ambayo mara nyingi hutoa huduma kwa kujitolea, yana upungufu wa fedha ambao umepunguza uwezo wao wa kukidhi mahitaji yaliyopo.

Mafuriko hayo yamechangiwa na mvua za wastani hadi nzito za wakati wa msimu wa mvua wa Gu unaoanza mwezi Aprili hadi Juni ambao mara nyingi huanzia tarehe 15 Aprili katika baadhi ya maeneo ya Somalia na nyanda za juu za Ethiopia, ambako mito ya Juba na Shabelle ndiko inakoanzia.