Je, kwa nini Trump amenyamazia kimya mauaji ya kimbari huko Gaza, huku akidai yametokea Afrika Kusini?
(last modified Fri, 23 May 2025 05:57:39 GMT )
May 23, 2025 05:57 UTC
  • Je, kwa nini Trump amenyamazia kimya mauaji ya kimbari huko Gaza, huku akidai yametokea Afrika Kusini?

Akizungumza siku ya Jumatano katika kikao chenye mvutano na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Rais Donald Trump wa Marekani alichukua hatua ya kushanga kwa kumuonyesha video ya kiongozi mmoja wa mrengo wa kulia wa Afrika Kusini aliyetoa wito wa kuuawa wakulima weupe ili kuthibitisha madai yake kuhusu kile kinachodaiwa kuwa mauaji ya kimbari dhidi ya wazungu wa nchi hiyo.

Katika hatua iliyopangwa awali huko White House, Trump alionyesha video hiyo kwa lengo la kudhalilisha na kumfanya Ramaphosa kuwa mlengwa wa mashambulizi yake ya maneno mbele ya kamera za televisheni. Alimkosoa vikali na kudai kuwa Afrika Kusini ilikuwa inaendesha "mauaji ya umati na kuwanyang'anya wazungu ardhi zao." Kwa maneno hayo ya kejeli na tuhuma zisizo na msingi, Trump alijaribu kuthibitisha madai ya uongo kuwa watu weupe hawalindwi vya kutosha na kuwa wananyimwa haki zao za msingi nchini Afrika Kusini. Tuhuma hizo dhidi ya Afrika Kusini ni jambo la kawaida kabisa katika utawala wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Marekani.

Ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kuboresha mahusiano yenye mvutano kati ya Marekani na Afrika Kusini na kujadili njia za kuimarisha uwekezaji, ushuru wa forodha na biashara ya malighafi. Uhusiano wa nchi hizi ulianza kuingia dosari baada ya utawala wa Trump kuweka ushuru, kuituhumu serikali ya Afrika Kusini kwa "mauaji ya halaiki ya wazungu," na kupendekeza kuwapa makazi Waafrikana ambao ni Waafrika Kusini wenye asili ya Uholanzi, nchini Marekani.

Baada ya kikao hicho, wengi walilinganisha hali hiyo na ile ya mvutano na ugomvi uliojitokeza kati ya Trump na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, na kuichukulia kuwa ni mbinu anayotumia Trump kwa ajili ya kuwashinikiza viongozi wa nchi dhaifu. Hata hivyo, mvutano uliozuka katika kikao cha Trump na Ramaphosa ulikuwa tofauti kwa kiasi fulani na ule wa Februari na Zelensky katika Ikulu ya White House. Inaonekana licha ya kuwa rais wa Afrika Kusini, hakutarajia pambano hilo la kisiasa, lakini alikuwa tayari kukabiliana nalo kwa namna fulani. Katika kikao hicho, alijaribu kukanusha madai ya Trump bila kukasirika, na wakati huo huo akikwepa ukosoaji wa moja kwa moja au makabiliano na Trump. Hata hivyo alimwambia kwa kejeli kwamba: "Samahani sina ndege ya kukupa kama zawadi." Matamshi hayo ya Ramaphosa yaliashiria hatua ya hivi karibuni ya serikali ya Qatar ya kumtunuku Trump ndege ambayo inatarajiwa kuwa ndege maalum ya Rais wa Marekani (Air Force One) katika siku zijazo.

Kikao chenye mvutano cha Marais wa Afrika kusini na Marekani White House

 

Tangu arejee Ikulu ya White House, Trump amekatiza misaada ya Marekani kwa Afrika Kusini, kumfukuza balozi wa nchi hiyo mjini Washington, na katika hatua ya kutatanisha, amewapa makazi Waafrikana walio wachache Afrika kusini haki ya kuwa wakimbizi katika ardhi ya Marekani. Hatua hii imekabiliwa na malalamiko makali kutoka mashirika ya wakimbizi na ya kijamii huko Marekani. Mvutano wa hivi karibuni wa kidiplomasia kati ya Marekani na Afrika Kusini ulianza kutokana na sheria mpya ya marekebisho ya ardhi nchini Afrika Kusini. Kwa mujibu wa viongozi wa Pretoria, sheria hiyo imebuniwa kwa ajili ya "kurekebisha dhuluma za enzi za ubaguzi wa rangi."

Nukta muhimu kuhusu hisia zisizo na muelekeo za Trump juu ya hali ya wazungu nchini Afrika Kusini, ambayo anadai ni mauaji ya halaiki, ni kwamba zinatokana na madai ya uwongo na yasiyo na msingi wowote. Huku akiwa anafahamu vizuri jinai kubwa zinazofanywa na Israel huko Gaza, hususan mauaji ya halaiki ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto wachanga wasio na hatia, ameamua kukaa kimya na kutosema lolote, hata kuonyesha masikitiko tu.

Kile Trump anachokiita  "mauaji ya halaiki" na "usafishaji wa kizazi" nchini Afrika Kusini ni kama tone la maji kwenye bahari ikilinganishwa na kile kilichofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha miezi ishirini iliyopita. Katika kipindi cha miaka minne ya karibuni, wakulima 225 wameuawa Afrika Kusini, 101 kati yao wakiwa ni watu weusi. Trump ameyaita mauaji hayo kuwa ya kimbari, huku akipuuza kabisa mauaji ya Wapalestina zaidi ya 52,000 huko Gaza tangu Oktoba 2023, na hata amekataa kueleza masikitiko yake kuhusu suala hilo. Isitoshe, ametuma shehena za kila aina ya silaha yakiwemo mabomu ya kisasa yenye uharibifu mkubwa kwa Israel ili iendeleze mauaji ya Wapalestina huko Gaza.
Suala hili kwa mara nyingine tena limeweka wazi siasa za kindumakuwili za Marekani kuhusu masuala muhimu ya kimataifa kama vile ugaidi, haki za binadamu na mauaji ya halaiki. Wakati maslahi ya Marekani na waitifaki wake kama vile Israel yanapokuwa hatarini, Marekani hufumbia macho kirahisi jinai zake zote na za utawala wa Kizayuni, huku ikichukua msimamo mkali inapokabiliana na nchi hasimu au adui, au nchi kama Afrika Kusini ambazo zimechukua misimamo thabiti dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni na kuushtaki utawala huo kwa kukiuka Mkataba wa Kimataifa wa Geneva unaopiga marufuku mauaji ya kimbari. Bila shaka, katika muktadha wa mauaji ya halaiki ya Wapalestina huko Gaza, Marekani inapaswa kuhesabiwa kuwa mshirika wa moja kwa moja wa Israel katika jinai hiyo isiyo na mfano wake kutokana na uungaji mkono wake mkubwa wa kisiasa, kidiplomasia, kijeshi na kiusalama kwa Tel Aviv, na vilevile kukandamizwa maandamano yanayopinga jinai hizo za Wazayuni ndani ya Marekani yenyewe.