Mkuu wa Jeshi la Uganda: US imeanzisha mazungumzo ya siri na al-Shabaab Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128328-mkuu_wa_jeshi_la_uganda_us_imeanzisha_mazungumzo_ya_siri_na_al_shabaab_somalia
Mkuu wa Jeshi la Uganda ametoa wito wa kuondolewa kikamilifu wanajeshi wa Umoja wa Afrika kutoka Somalia, akidai kuwa Marekani imeanzisha mazungumzo ya siri na kundi la kigaidi la al-Shabaab.
(last modified 2026-05-10T14:24:40+00:00 )
Jul 14, 2025 11:03 UTC
  • Mkuu wa Jeshi la Uganda: US imeanzisha mazungumzo ya siri na al-Shabaab Somalia

Mkuu wa Jeshi la Uganda ametoa wito wa kuondolewa kikamilifu wanajeshi wa Umoja wa Afrika kutoka Somalia, akidai kuwa Marekani imeanzisha mazungumzo ya siri na kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Tovuti ya habari ya Garowe ya Somalia iliandika habari hiyo jana Jumatatu, ambapo imemnukuu Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda (UPDF) ambaye pia na mtoto wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda akitoa mwito wa kuondoka vikosi hivyo vya AU, vikiwemo vya Uganda nchini Somalia.

Kainerugaba amedai kuwa, Marekani imeanzisha mazungumzo ya siri na kundi la wanamgambo la al-Shabaab, na kuhujumu juhudi za vikosi vya kulinda amani vya Kiafrika nchini Somalia (AUSSOM). 

"Marekani na mataifa ya Magharibi yanaitambua Al Qaeda nchini Syria. Hata Israel wanaonekana kuwa sawa na hali hii?" Kainerugaba amehoji.

Mkuu wa UPDF ameeleza bayana kuwa, "Hata tunasikia kwamba Marekani imeanza mazungumzo ya siri na al-Shabaab nchini Somalia. Tutamwomba Amiri Jeshi Mkuu kufikiria kujiondoa kabisa Somalia baada ya (kuwepo nchini humo kwa) miaka 18."

Wanajeshi wa Uganda wamekuwa sehemu kuu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia. Tangu mwaka 2007, Uganda imechangia maelfu ya wanajeshi katika misheni hiyo, ambayo inalenga kuleta utulivu nchini humo na kupambana na uasi wa al-Shabaab wenye mfungamano na al-Qaeda.

Licha ya takriban miongo miwili ya operesheni za kijeshi, lakini al-Shabaab bado ni genge la kutisha, linaloendelea kufanya mashambulizi mabaya nchini Somalia na katika eneo zima.