27 wauawa katika shambulio la watu wenye silaha katika jimbo la Plateau, Nigeria
Watu wasiopungua 27 wameuawa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha kaskazini kati mwa jimbo la Nigeria la Plateau, katika machafuko ya hivi karibuni yaliyolikumba eneo hilo ambalo halina usalama wa kutosha.
Jimbo la Plateau, kama yalivyo baadhi ya maeneo mengine nchini Nigeria, limekuwa likishuhudia mapigano kati ya wakulima na wafugaji wanaogombania ardhi na maliasili pamoja na machafuko yanayosababishwa na magenge ya wahalifu.
Mkazi mmoja Haggai Gankis amevieleza vyombo vya habari kuwa washambuliaji walikwenda kwenye eneo la Jebu-Rahoss, siku ya Jumatatu jioni, wakiwa na bunduki na mapanga.
Akisimulia alivyoshuhudia hujuma hiyo, Chuwang David amesema: tulikuwa tumelala usiku, tukaskia milio ya risasi, washambuliaji walipiga risasi watu wengi sana na pia walitumia mapanga".
Mkazi mwingine wa eneo hilo Da Chomo Moses ameeleza kwamba yeye alipoteza wanafamilia watatu.
"Watu ishirini na saba ambao hawakuwa na hatia waliuawa kwa risasi," alisema Gankis, akiongeza kuwa wengi wao walikuwa wanawake.
Wakazi wa eneo hilo wamevieleza vyombo vya habari kwamba, kuna idadi isiyojulikana ya watu ambao walipelekwa hospitali.
Kwa miaka kadhaa, mashambulizi ya watu wenye silaha yameongezeka vijijini kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria.
Katika mwezi Aprili pekee, mashambulizi yaliyofanywa kote katika jimbo la Plateau na jimbo la jirani la Benue yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 150.
Machafuko mengi katika jimbo la Plateau yanatokea kwenye maeneo ambayo kuna polisi wachache.../