Watoto wanakufa kwa njaa katika jimbo la Darfur, Sudan huku ugonjwa wa Kipindupindu ukienea
Watoto 13 wameaga dunia kutokana na njaa katika kambi ya raia waliokimbia makazi yao katika jimbo la Darfur Mashariki nchini Sudan.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa janga la ugonjwa wa kipindupindu limeenea katika maeneo mengine ya jimbo la Darfur Mashariki lililoathiriwa na vita.
Vifo hivyo vya watoto vimetokea katika kambi ya Lagawa katika mji wa al Daein huko Darfur Mashariki inayodhibitiwa na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Mzozo unaoendelea kati ya RSF na jeshi la Sudan umelemaza utoaji wa misaada ya kibinadamu na kuwaacha watu waliokimbia makazi yao wakiwa katika hatari ya njaa na magonjwa.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umearifu kuwa, kambi ya Lagawa inawahifadhi watu 7,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto ambao hawana misaada muhimu.
Mtandao huo umetoa wito wa kuchukuliwa hatua mara moja ili kuwapatia chakula, huduma ya afya na kulinda kambi za wakimbizi dhidi ya mashambulizi ya makundi yenye silaha.
Wakati huo huo, Adam Ragal, msemaji wa Zoezi la Uratibu wa Wakimbizi amesema kuwa mlipuko wa ugonjwa kipindupindu umeenea kwa kiwango cha "kutisha" katika kambi za wakimbizi za kusini, kaskazini na Darfur ya Kati huko Sudan.