AU yatoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa kushughulikia mgogoro wa Mali
-
AU: Jamii ya Kimataifa ishughulikie hali ya Mali
Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssef, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa kasi hali ya usalama nchini Mali, ambako makundi aliyoyataja kuwa ya "kigaidi" yamezuia operesheni za kuwasilisha mahitaji ya msingi na hivyo kuzidisha mgogoro wa binadamu unaowakabili raia, pamoja na kuongezeka kwa utekaji nyara.
Katika taarifa yake, Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika amelaani mashambulizi yanayowalenga raia, ambayo yamesababisha vifo na kuzidisha ukosefu wa amani nchini Mali, akitaka uingiliaji kati wa haraka wa kimataifa ili kupambana na "ugaidi na itikadi kali".
Umoja wa Afrika umesisitiza mshikamano wake kamili na serikali, watu wa Mali na familia za waathiriwa, ukitilia mkazo azma yake ya dhati na kusaidia juhudi za amani, usalama na maendeleo katika eneo la Sahel.
Mahmoud Ali Youssef pia amelaani utekaji nyara wa hivi karibuni, akitaka kuachiliwa huru mara moja na bila masharti watu waliotekwa nyara, na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua ya haraka na iliyoratibiwa ya kimataifa ya kupambana na ugaidi na msimamo mkali katika eneo la Sahel.
Vilevile ametangaza utayarifu wa Umoja wa Afrika wa kutoa msaada wowote unaohitajika ili kuimarisha juhudi za Mali na nchi zingine za Sahel za kurejesha amani na utulivu.
Kwa wiki kadhaa sasa makundi ya kigaidi yenye mfungamano na mtandao wa al Qaida yamekuwa yakivuruga usambazaji wa mafuta nchini Mali na kusababisha mgogoro mkubwa kwa baraza tawala la kijeshi. Makundi hayo pia yamezidisha vitendo vya kuteka nyara watu hasa katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.