Hatari ya ushawishi wa Israel barani Afrika; Tishio lililofichika kwa uhuru wa bara Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133024-hatari_ya_ushawishi_wa_israel_barani_afrika_tishio_lililofichika_kwa_uhuru_wa_bara_afrika
Katika juhudi zake za kuitoa Israel kwenye hali ya kutengwa, Isaac Herzog, rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel, anatarajiwa kuelekea barani Afrika.
(last modified 2025-11-10T13:05:19+00:00 )
Nov 10, 2025 13:05 UTC
  • Hatari ya ushawishi wa Israel barani Afrika; Tishio lililofichika kwa uhuru wa bara Afrika

Katika juhudi zake za kuitoa Israel kwenye hali ya kutengwa, Isaac Herzog, rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel, anatarajiwa kuelekea barani Afrika.

Katika juhudi zake za kuiondoa Israel kwenye hali ya kutengwa, Isaac Herzog, rais wa utawala wa Kizayuni, anatarajiwa kuelekea barani Afrika.

Herzog, katika harakati za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya utawala wa Kizayuni na baadhi ya mataifa ya Afrika, atafanya ziara nchini Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanzia siku ya Jumatatu, tarehe 10 Novemba. Ziara hii inakuja wakati ambao Israel iko katika upweke mkubwa wa kimataifa, ikikabiliwa na hasira ya fikra za ulimwengu kutokana na vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina Gaza na siasa zake za uvamizi. Hivyo basi, uingiliaji wa Israel barani Afrika si mradi wa kawaida wa kidiplomasia; ni mapambano ya kujinasua kisiasa na kuchora upya sura yake mbele ya dunia baada ya miaka mingi ya lawama, shutuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, na upinzani wa kimataifa. Hakuna shaka kuwa Israel inaendelea kutengwa kutokana na jinai zake dhidi ya Wapelestina hasa wa Gaza.

Umuhimu wa Afrika kwa Tel Aviv hauishii kwenye uchumi pekee. Bara hili lina kura zaidi ya hamsini katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lina utajiri wa madini, masoko yanayokua, na mataifa mengi yanayohitaji uwekezaji wa nje, nukta ambazo Israel inaziona kama fursa za kimkakati. Kwa mtazamo wa Tel Aviv, kila mkataba wa kilimo, teknolojia au ulinzi si biashara tu, bali ni akiba ya kisiasa, akiba inayoweza kutumika kupunguza mawimbi ya shutuma katika majukwaa ya kimataifa.

Kwa sababu mataifa mengi ya Afrika yanategemea uwekezaji wa nje kwa maendeleo, Israel inajaribu kutumia nafasi hiyo kupunguza hali yake ya kutengwa. Kwa nje, Tel Aviv hujionyesha kama mshirika wa maendeleo kupitia miradi ya kilimo, maji, vifaa vya ulinzi, mafunzo ya usalama, uchimbaji madini na ushirikiano wa kijasusi. Hata hivyo, hali halisi inaonyesha malengo ya ndani yanayokwenda mbali zaidi, kuongeza utegemezi, kupata uhalali wa kisiasa, na kuitumia Afrika kama kinga ya kidiplomasia dhidi ya mashinikizo ya dunia. Hata pale baadhi ya serikali za Afrika zinapodumisha mahusiano na Israel, mara nyingi si kwa misingi ya mapenzi ya kisiasa, bali kwa matarajio ya kupata mikopo, misaada, au ushirikiano wa  kijeshi.

Pamoja na hayo, sehemu kubwa ya viongozi wa kisiasa, wanaharakati, na jamii za kiraia barani Afrika wanapinga uhusiano wa nchi zao na utawala haramu wa Isarel.

Maandamano dhidi ya utawala haramu wa Israel, Mombasa , Kenya

Kumbukumbu za ukatili wa ukoloni, uporaji wa rasilimali, na matumizi ya Afrika kama eneo la majaribio bado ziko hai katika fikra za watu wengi. Aidha, tangu kupambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, upinzani dhidi ya siasa za kibaguzi umekuwa sehemu ya utu na utambulisho wa kisiasa wa Afrika. Ndiyo maana utawala wa Kizayuni—unaotajwa na mashirika ya haki za binadamu na ripoti za Umoja wa Mataifa kama mfumo wa ubaguzi na utawala wa kikoloni, hauwezi kupokewa kwa shangwe barani Afrika.

Makundi mengi ya kisiasa barani Afrika huchukulia uwepo wa Israel kama mwendelezo wa mantiki ile ile ya zamani: nguvu ya nje inaingia kwa jina la “maendeleo”, lakini mwisho wa siku inanufaika yenyewe baada ya kupora utajiri wa bara hilo. Pia kuna hofu kubwa kuwa teknolojia za usalama na ujasusi zinazotolewa na Israel zitaishia kutumika kwa ukandamizaji wa kisiasa ndani ya baadhi ya mataifa ya Afrika, badala ya maendeleo ya watu. Mfano halisi ni jitihada za Israel kujipatia hadhi ya  mwanachama “mwangalizi” ndani ya Umoja wa Afrika, hatua iliyozua msuguano mkubwa na upinzani mkali, kwa sababu mataifa mengi yaliona hatua hiyo kama kupuuza historia ya mshikamano wa Afrika na Palestina, na kuacha kupinga ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kwa upande wa wananchi, hisia za Wafrika zimejaa mshikamano na Wapalestina. Ndiyo maana katika vita vya Gaza, Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza kuifungulia Israel kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ikiishtaki kwa kukiuka Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari wa 1948, na mataifa mengine ya Afrika yakafuata mkondo huo.

Lengo jingine la Israel katika upanuzi wa mahusiano yake barani Afrika ni kujenga ukuta wa diplomasia ili kujilinda dhidi ya shinikizo la dunia. Lakini kama mataifa ya Afrika yanataka kulinda uhuru wao wa kweli, ni lazima yatambue kwamba nyuma ya tabasamu za kisiasa na miradi midogo ya “msaada wa kiufundi”, mara nyingi pana hesabu nzito za kisiasa na kiusalama.

Afrika leo inahitaji washirika wanaoheshimu utu, uhuru na maendeleo endelevu na si uhusiano unaomalizika kwenye utegemezi na unyonyaji wa rasilimali. Bara hili lina historia ya mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi. Kwa msingi huo, kukubali utawala unaoendeleza uvamizi na ubaguzi dhidi ya Wapalestina, kunapingana na urithi wa ukombozi wa Afrika.

Ikiwa bara Afrika linataka kubaki mwaminifu kwa historia yake ya fahari, basi ni jukumu lake kuendelea kusimama imara dhidi ya mkakati wa utawala wa kibaguzi wa Israel wa kutaka kujipatia uhalali katika uga wa kimataifa.

Kuziba mianya ya ushawishi huo ni mwendelezo wa safari ile ile iliyolinda uhuru, heshima na mshikamano wa mataifa ya Afrika.