Mfuasi wa zamani wa Mchungaji Mackenzie: Nilitoa tahadhari kuhusu mauaji ya Shakahola, sikusikilizwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133080-mfuasi_wa_zamani_wa_mchungaji_mackenzie_nilitoa_tahadhari_kuhusu_mauaji_ya_shakahola_sikusikilizwa
Aliyekuwa mfuasi wa Mchungaji Paul Mackenzie, kiongozi wa Kanisa la Good News International (GNI) amefichua jinsi alivyotoa onya kuhusu mauaji ya Shakahola lakini hakusiikilizwa na vyombo husika.
(last modified 2025-11-12T07:33:43+00:00 )
Nov 12, 2025 07:33 UTC
  • Mamia waliuawa Shakahola
    Mamia waliuawa Shakahola

Aliyekuwa mfuasi wa Mchungaji Paul Mackenzie, kiongozi wa Kanisa la Good News International (GNI) amefichua jinsi alivyotoa onya kuhusu mauaji ya Shakahola lakini hakusiikilizwa na vyombo husika.

Bi Brenda Mwaura, aliyekuwa mshiriki wa kanisa hilo na mfuasi wa mhubiri huyo, alitoa maelezo jana kuhusu alivyotoa tahadhari mapema kuhusu hatari ya mauaji ya Shakahola alipokuwa akitoa ushahidi mbele ya mahakama ya Mombasa.

“Nilichoshwa na mafundisho tata ya pasta Paul Mackenzie kuhusu mwisho wa dunia. Niliona maafa yakija,” amesema 

Bi Mwaura, ambaye sasa anajulikana kama mlalamikaji mkuu katika kesi hiyo, hakuwa mshiriki wa kawaida bali alikuwa mhusika muhimu katika kurekodi, kuhariri na kusambaza mahubiri ya Mackenzie kupitia kituo cha Times TV kwa mauzo kwa waumini na watu wengine waliovutiwa na mafundisho yake.

Katika chapisho lake la Facebook mwezi Novemba 2022, miezi minne tu kabla ya mauaji ya Shakahola kufichuliwa, alidai kuwa Mackenzie alikuwa “akiwaua watu na kuwazika kwenye shamba lake.” Alimtaja pia Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) akitaka achukue hatua, lakini hakuna kilichofanyiika.

“Sikupuuza onyo hilo. Nilipata habari kutoka kwa baba yangu kwamba watu walikuwa wanakufa kule shambani. Aliniambia Mackenzie anaua watu. Watu hawakuruhusiwa kuondoka,” alisema Bi Mwaura.

Baba yake, ambaye alikuwa mhubiri wa zamani wa GNI na pia alikuwa akisafirisha maua kutoka Nairobi hadi Shakahola, alikosana na Mackenzie kutokana na tofauti za kiimani.

“Nilichopata tu ni vitisho kutoka kwa watu wa Mackenzie,” alisema Bi Mwaura na kuongeza: “Waliniambia sijui nilichokuwa nikichapisha na kwamba wangenifuata.” 

Shahidi huyo wa mauaji ya kutisha ya Shakahola amesema: “Sikuitikia wito wa polisi kwa sababu niliogopa huenda ningekuwa mhanga wa kuwekwa kizuizini au kupotea.” 

Akihojiwa na wakili wa Mackenzie, Bi Mwaura alisema baba yake alijiondoa kanisa la Mackenzie “alipoanza kuwaua watu,” akiongeza: “Alikuwa anatoa maagizo kwa wafuasi wake watekeleze ‘kazi hiyo’ kwa niaba yake.”

Mchungaji Paul Mackenzie na wafuasi wake kadhaa walikamatwa mwaka juzi mwezi Aprili na wamekuwa kizuizini tangu wakati huo ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.

Paul Mackenzie na wenzake wakiwa kizimbani

Miili ya watu 450 wakiwemo watoto imefukuliwa kutoka maeneo ya makaburi huko Shakahola na uchunguzi umebaini kuwa mbali na kufa kwa njaa, wengine waliuawa kwa kunyongwa.

 Kiongozi wa Kanisa la Good News International na wenzake wanatuhumiwa kusababisha vifo vya mamia ya watu kwa kuwaamuru wajizuiye kula chakula hadi wafe kwa njaa ili waweze kukutana na Yesu Kristo huko mbinguni!