Shirika la Umoja wa Mataifa: Kuna Ushahidi wa matumizi ya kimfumo ya ubakaji nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133084-shirika_la_umoja_wa_mataifa_kuna_ushahidi_wa_matumizi_ya_kimfumo_ya_ubakaji_nchini_sudan
Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wanawake limeonya kwamba kuna "ushahidi unaoongezeka kwamba ubakaji unatumika kwa makusudi na kwa utaratibu maalumu" nchini Sudan, huku njaa na ukosefu wa usalama wa chakula vikiendelea kutesa watu nchini humo.
(last modified 2025-11-12T07:39:24+00:00 )
Nov 12, 2025 07:39 UTC
  • UN: Wanawake wanabakwa kimfumo El Fasher
    UN: Wanawake wanabakwa kimfumo El Fasher

Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wanawake limeonya kwamba kuna "ushahidi unaoongezeka kwamba ubakaji unatumika kwa makusudi na kwa utaratibu maalumu" nchini Sudan, huku njaa na ukosefu wa usalama wa chakula vikiendelea kutesa watu nchini humo.

Anna Mutavati, mkurugenzi wa kikanda wa shirika hilo kwa Afrika Mashariki na Kusini, ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari huko Geneva na kuongeza kuwa: "Kila siku dunia inapochelewe kuchukua hatua, mwanamke mmoja hujifungua chini ya mashambulizi ya mabomu, au humzika mtoto wake kutokana na njaa, au hutoweka bila haki."

Mutavati ameongeza kuwa ushahidi uliotolewa na wanawake katika mji wa El Fasher - ambao ameutaja kuwa ni "kitovu cha janga la hivi karibuni nchini Sudan" - umefichua mateso ya kutisha.

Amesema kuwa "wanawake wajawazito wamelazimika kujifungulia mitaani baada ya hospitali ya mwisho ya uzazi katika mjini huo kuharibiwa na kuporwa."

Ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu zimesema Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) viliudhibiti mji wa El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, mwishoni mwa Oktoba, na kufanya "ukatili mkubwa ikiwa ni pamoja na mauaji ya papo hapo na unyanyasaji wa kingono".

Uhalifu huo, kama anavyosema Anna Mutavati, umelazimisha maelfu ya wanawake na wasichana kukimbilia maeneo ya Tawila, Korma na Mellit, yapata umbali wa kilomita 70 kutoka El Fasher.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba "miili ya wanawake imekuwa uwanja wa uhalifu nchini Sudan," akionya kwamba "hakuna sehemu salama" zilizobaki ambapo wanawake wanaweza kupata ulinzi au msaada wa kisaikolojia na kijamii. 

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kukomeshwa mara moja ukatili huo, kupanuliwa zaidi operesheni za misaada ya kibinadamu, na kuongeza ufadhili kwa mipango ya ndani inayoongozwa na wanawake.