Mudavadi: Zaidi ya Wakenya 200 wanapigana pamoja na Russia katika vita vya Ukraine
-
Musalia Mudavadi
Serikali ya Kenya imesema kwamba zaidi ya raia wake 200 wanapigana katika safu ya jeshi la Russia katika vita vyake dhidi ya Ukraine, ikionya kwamba mitandao ya kuajiri wapiganaji bado inaendelea kufanya kazi na inawalenga Wakenya kwa kutoa kazi zenye kipato kikubwa.
Kinara wa Mawaziri wa Kenya ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi, ameeleza katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya wizara hiyo kwamba "ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya Wakenya 200 huenda wamejiunga na jeshi la Russia, baadhi yao wakiwa wanachama wa zamani wa vyombo vya usalama vya Kenya."
Ukraine ilitangaza wiki iliyopita kwamba zaidi ya raia 1,400 kutoka takriban nchi 30 za Afrika wanapigana pamoja na vikosi vya jeshi la Russia, ikieleza kwamba baadhi yao waliajiriwa kwa njia za udanganyifu.
Modavadi ameitaja hali hiyo kuwa "ya kutisha sana," akiwahimiza raia kuwa waangalifu na ofa za kazi za nje ya nchi ambazo zinaonekana kuwa zisizo za kweli au za kuvutia kupita kiasi.
Itakumbukwa kwamba wiki iliyopita, Rais wa Kenya, William Ruto alimpigia simu mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ambapo aliomba kuachiliwa Wakenya wanaozuiliwa katika maeneo yenye migogoro.
Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini pia ilitangaza mnamo Novemba 6 kwamba juhudi za kidiplomasia zinaendelea kwa ajili ya kuwarudisha nyumbani raia 17 ambao walishawishiwa kujiunga na mapigano huko Ukraine kama mamluki mkabala wa ahadi za mishahara mikubwa, kabla ya kutelekezwa kwenye uwanja wa mapigano katika eneo la Donbas, mashariki mwa Ukraine.
Matukio haya yanaangazia suala la kuajiriwa Waafrika katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine, ama kutokana na mahitaji ya kiuchumi au ahadi za kupotosha, jambo ambalo linazidisha wasiwasi miongoni mwa serikali za nchi za Afrika kuhusu athari mbaya za kiusalama na kijamii za muda mrefu.