Bunge la Tanzania lamthibitisha Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo
-
Mwigulu Nchemba
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Alhamisi limemthibitisha Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo baada ya kupata kura 369 kati ya kura 371 zilizopigwa na wabunge. Baada ya uthibitisho huo, Dkt. Nchemba ataapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuanza mara moja majukumu yake.
Rais Samia Suluhu Hassan mapema leo aliwasilisha bungeni jina la Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu mpya wa serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Spika Mussa Zungu alipokea hati ya uteuzi huo kutoka kwa Rais Samia na kulitangaza kwa wabunge kwa ajili ya kumthibitisha kwa kura, kwa mujibu wa Ibara ya 51 kifungu kidogo cha pili.
Baada ya kuthibitishwa na wabunge kwa kura nyingi, Dakt Nchemba ametoa hotuba bungeni ambapo amesema kuwa katika wadhifa wake huo mypa atahakikisha kuwa kila Mtanzania anahudumiwa kwa heshima katika taasisi za serikali na kwamba wavivu wote na watumishi wa umma wenye kauli mbovu kwa Watanzania watashughulikiwa.
"Mimi umaskini wa Watanzania sijausoma kwenye vitabu, nimeuishi. Mheshimiwa Spika katika maisha yangu haya ya umri wangu huu, miaka takribani 32 nimeishi katika maisha hayo ya umaskini."
Amesema: "Watumishi wa Umma na Watanzania wote lazima twende kwa gia ya kupandia mlima, lazima twende na gia ya kupita kwenye bahari yenye mawimbi na anga lenye mawingu ili chombo kifike salama na watu wake wakiwa salama."
Mwigulu anakuwa Waziri Mkuu wa 12 tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.
Mwigulu ni mchumi, kada wa muda mrefu wa chama cha mapinduzi (CCM) akimrithi Kassim Majaliwa anayemaliza muda wake. Mwanasiasa huyo wa muda mrefu, alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango.