Kwa nini kutoshiriki Marekani katika kikao cha G20 nchini Afrika Kusini ni hasara kubwa kwa Washington?
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa kutohudhuria Wamarekani katika kikao cha G20 ni hasara kubwa kwao.
Akijibu tishio la Rais Donald Trump wa Marekani kwamba maafisa wa nchi yake hawatahudhuria kikao hicho mjini Johannesburg, Rais Ramaphosa, alisema Jumatano kwamba kususia Marekani mkutano wa kilele wa G20 uliopangwa kufanyika Novemba 22-23 huko Johannesburg, Afrika Kusini, hakutazuia kufanyika mkutano huo wa nchi zinazoongoza kiuchumi duniani. Alisisitiza kwa kusema: "Tutafanya maamuzi ya msingi na kutokuwepo kwao kunamaanisha hasara kwao. Washington inakwepa kutekeleza jukumu muhimu ambalo inapaswa kulitekeleza kama uchumi mkubwa zaidi duniani."
Akizungumzia mkutano ujao wa Kundi la G20, Rais Trump amedai kuwa mkutano huo ni wa aibu na kwamba hakuna afisa wa serikali yake atakayehudhuria. Trump alidai katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social kwamba: "Waafrikana" nchini Afrika Kusini wanauawa kwa umati na ardhi na mashamba yao yamechukuliwa kinyume cha sheria. Kwa mujibu wa Trump, Afrika Kusini haipaswi kuwa mwanachama wa G20 na inapaswa kuondolewa kwenye kundi hili. Huku akidai kuwa maadamu ukiukaji huu wa haki za binadamu unaendelea nchini Afrika Kusini, hakuna afisa wa serikali yake atakayeshiriki katika mkutano wa G20 unaoandaliwa na nchi hii, amesema: Ninasubiri kwa hamu kuandaa mkutano wa G20 huko Miami, Florida mnamo 2026.
Kama alivyosema rais wa Afrika Kusini, kutoshiriki Marekani katika mkutano wa G20 huko Johannesburg kunachukuliwa kuwa kushindwa kimkakati Washington kwa sababu hatua hii itadhoofisha itibari yake ya kimataifa, kupunguza ushawishi wake wa kidiplomasia na kuwaandalia uwanja wapinzani wake wa kijiopolitiki kama vile China na Russia.
Mkutano wa G20 ni mojawapo ya majukwaa muhimu ya kimataifa ya kufanya maamuzi kuhusu masuala ya kiuchumi, mazingira na kijiografia duniani. Katika mkutano huu, mataifa makubwa na yenye uchumi unaoinukia yatakutana ili kujadili changamoto zinazofanana na kuwasilisha masuluhisho yaliyoratibiwa. Kutokuwepo kwa Marekani katika mkutano wa G20 mjini Johannesburg, kunakotimia kwa kisingizio cha tofauti za kisiasa na serikali ya Afrika Kusini, kuna madhara makubwa kwa Washington.
Kwanza, kutohudhuria huku ni kurudi nyuma na kupuuza diplomasia ya pande kadhaa kimataifa. Marekani daima imejaribu kuchukua nafasi ya uongozi katika taasisi za kimataifa. Kukataa kuhudhuria mkutano huo muhimu, tena kwa sababu za kisiasa, kunaonyesha kupungua kwa uwajibikaji wa Washington katika ushirikiano wa kimataifa. Hili linaweza kupunguza imani ya washirika wake kuhusu uwajibikaji wake na hivyo kuwa msingi wa nchi nyingi za kusini mwa dunia kuamua kuwa na ushirikiano wa karibu na nchi nyingine zenye nguvu kubwa duniani kama China na Russia.
Pili, kama bara lenye ukuaji wa haraka wa uchumi na maliasili tajiri, Afrika ina umuhimu mkubwa wa kijiografia. Mkutano wa G20 nchini Afrika Kusini ni fursa ya kutangamana moja kwa moja na viongozi wa Afrika na kuimarisha nao uhusiano wa kiuchumi na kisiasa. Kutoshiriki Marekani katika kikao hicho kunamaanisha kutoa fursa hii kwa washindani wake wa kimkakati. China, ambayo ina uwepo hai barani Afrika, itatumia fursa ya ombwe hili kwa madhumuni ya kupanua ushawishi wake barani humo. Pia, hii inachukuliwa kuwa fursa nzuri kwa Russia kupanua ushawishi wake barani Afrika.
Tatu, katika hali ambayo dunia inakabiliwa na matatizo makubwa kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa chakula na ukosefu wa usawa wa kiuchumi, kutoshiriki Marekani katika kufanya maamuzi ya pamoja kunadhoofisha juhudi za kimataifa za kutatua migogoro hii. Kama taifa kubwa kiuchumi duniani, Marekani ina jukumu muhimu katika kuchangia rasilimali, teknolojia na ufumbuzi wa sera kwa mataifa mengine. Kutoshiriki katika mkutano wa G20 kunamaanisha kujiondoa kwenye uwajibikaji wa kimataifa.
Nne, kwa mtazamo wa ndani pia, uamuzi huu unaweza kupelekea kukosolewa siasa za kigeni za utawala wa Trump. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa vitendo kama hivyo vinaimarisha taswira ya Marekani kuonekana kama nchi iliyotengwa na isiyo na ushirikiano wa kimataifa. Hili linaweza kuathiri vibaya mahusiano ya kibiashara, uwekezaji wa kigeni na hata nafasi ya dola katika mfumo wa fedha duniani.
Hatimaye, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, katika kujibu kutowajibika huko kwa Marekani amesema kwamba uamuzi huu ni hasara kwa nchi hiyo ya Magharibi na kwamba mkutano huo utafanyika na kuchukua maamuzi muhimu yanayohitajika hata bila uwepo wa Washington. Msimamo huu unaonyesha kwamba ulimwengu unaelekea kwenye utaratibu wa kambi kadhaa za uchukuaji maamuzi na kuwa kutokuwepo kwa Marekani sio tu hakutazuia maendeleo, bali kutaharakisha mchakato huu.
Inaonekana kuwa kutoshiriki Marekani katika kikao cha G20 sio kitendo cha kawaida cha makosa ya kisiasa, bali ni kosa la kimkakati ambalo matokeo yake ya muda mrefu bila shaka yataathiri pakubwa nafasi yake ya kimataifa.