Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo DR: Rwanda lazima ionyeshe hamu ya kweli ya kutaka amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133168-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_congo_dr_rwanda_lazima_ionyeshe_hamu_ya_kweli_ya_kutaka_amani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Thérèse Kayikwamba Wagner, ameikosoa vikali Rwanda, akiitaka ithibitishe dhamira yake ya kweli ya kutaka amani, kutokana na uwepo wa vikosi vyake ndani ya ardhi ya Congo na mvutano unaoongezeka mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2025-11-14T10:14:24+00:00 )
Nov 14, 2025 10:14 UTC
  • Thérèse Kayikwamba Wagner akihojiwa
    Thérèse Kayikwamba Wagner akihojiwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Thérèse Kayikwamba Wagner, ameikosoa vikali Rwanda, akiitaka ithibitishe dhamira yake ya kweli ya kutaka amani, kutokana na uwepo wa vikosi vyake ndani ya ardhi ya Congo na mvutano unaoongezeka mashariki mwa nchi hiyo.

Kayikwamba Wagner ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar. Amesema vitendo vya Rwanda vinaibua shaka kuhusu nia yake ya kushiriki katika mchakato wa amani unaolenga kukomesha miongo kadhaa ya migogoro mashariki mwa Congo. 

Ameongeza kuwa mkutano uliokuwa umepangwa baina ya marais wa nchi hizo mbili bado umesitishwa, huku ukiukwaji wa makubaliano ya kusitishwa vita mashariki mwa Congo DR ukiendelea licha ya juhudi za kidiplomasia.

Thérèse Kayikwamba Wagner amesisitiza kuwa kupatikana maendeleo halisi kunahitaji mashinikizo ya kweli ya wapatanishi wa kimataifa na washirika wa kikanda, ili kuhakikisha kwamba pande zote mbili zinawajibika na kusukuma mbele mchakato kuelekea kwenye makubaliano ya kuaminika na endelevu.

Wagner amedai kwamba serikali ya Congo ina ushahidi usiopingika wa uungaji mkono wa Rwanda kwa harakati ya waasi ya "M23" ambayo inavuruga utulivu wa eneo la Kivu Kaskazini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kwamba msaada huo hauishii katika ufadhili na kuwapa silaha, lakini pia unajumuisha uratibu wa moja kwa moja wa kijeshi, akieleza kuwa uwepo wa vikosi vya jeshi la Rwanda ndani ya ardhi ya Congo unawakilisha ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya kitaifa.

Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetoa mapendekezo ya wazi ya kusitisha mapigano na kuondolewa vikosi vya kigeni mashariki mwa nchi, lakini upande wa Rwanda haukuyaheshimu, jambo linalozua shaka kuhusu nia yake ya kweli.

Waziri Kayikwamba Wagner ameashiria taathira za kikanda za mzozo huo na kusema, ukosefu wa amani mashariki mwa Congo unaathiri usalama katika eneo lote la Maziwa Makuu.

Wakimbizi wa ndani, Congo DR

Vilevile ameangazia hali mbaya ya binadamu mashariki mwa nchi, ambapo mapigano yamelazimisha mamia ya maelfu ya raia kukimbia makazi yao na kuzidisha mgogoro wa chakula na huduma za msingi.