Rais wa Tanzania atoa msamaha kwa vijana waliofanya fujo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu
Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa vijana waliofanya fujo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 akisema kuwa, walifuata mkumbo na hawakujua walifanyalo.
Rais Samia ametoa maelekezo maalumu kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, hususan Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuchuja upya mashitaka yanayowakabili vijana walioshtakiwa kwa makosa ya uhaini kufuatia fujo zilizofanyika wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 nchini humo.
Akihutubia Bunge jana Ijumaa, Novemba 14, 2025, jijini Dodoma, Rais Samia amesema kuwa, serikali yake inatambua kwamba kati ya vijana waliokamatwa, wapo waliojiingiza katika fujo hizo kufuata mkumbo bila ya kufahamu uzito wa matendo yao, hivyo hawakudhamiria kufanya uhalifu.
Katika sehemu moja ya matamshi yake, Rais Samia amesema: “Ninatambua kuna vijana wengi wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini. Wengine hawakujua wanachokifanya, na wengine walifuata mkumbo tu. Nikiwa kama Mama, naelekeza vyombo vya kisheria kuangalia kwa makini makosa yaliyofanywa na vijana wetu. Kwa wale ambao walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wawafutie makosa yao.”
Aidha amesema: “Ukiangalia zile clip, unaona vijana wanaingia kwa kufuata mkumbo, wanaimba kwa ushabiki. Naelekeza Ofisi ya DPP kuchuja viwango vya makosa. Wale walioingia bila ya nia ya kufanya uhalifu waachwe waende kwa wazazi wao.”
Kauli hiyo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonekana kutoa matumaini mapya kwa familia na makundi ya vijana waliokumbwa na operesheni za usalama baada ya ghasia hizo, sambamba na kuonesha msimamo wa serikali ya Tanzania wa kulinda sheria bila ya kuwaumiza wasio na dhamira mbaya.