Serikali ya Kongo yatoa hakikisho; yasema haitasalimu amri licha ya hali ya wasiwasi mashariki mwa nchi
-
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana Ijumaa ilitoa hakikisho ikieleza kuwa jeshi la nchi hiyo halitasalimu amri" kufuatia kutekwa mji wa Uvira.
Guillaume Ngefa Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameeleza haya ikiwa imepita siku kadhaa baada ya waasi wa M23 kuteka kitovu muhimu cha kibiashara katika jimbo la Kivu Kusini mashariki mwa nchi hiyo karibu na mpaka na Burundi, bila kukabiliwa na upinzani wowote.
Waziri wa Sheria wa Kongo amekutana na mabalozi na wanadiplomasia kadhaa na kusisitiza kuhusu azma ya serikali ya nchi hiyo ya kulinda umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo.
Ngefa ameahidi kuwa mji wa kimkakati wa Uvira utadhibitiwa tena na vikosi vya serikali. Ameongeza kuwa: "Msimamo wa serikali ya Kongo uko wazi na wa kuwajibika. Awali ya yote ni kuwa, hatusalimu amri. Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vikiungwa mkono na vikosi vya washirika vinajipanga upya ili kulinda mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya Kongo".
Mapigano yameshtadi katika maeneo kadhaa ya Kivu Kusini siku chache zilizopita baada ya Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mwenzake wa RwandaPaul Kagame kutia saini makubaliano ya amani na kiuchumi ili kukomesha mapigano mashariki mwa Kongo.
Kumekuwa na shutuma nyingi, huku kila upande ukilaumu upande mwingine kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano kwa mujibu wa mkataba wa amani uliosimamiwa na Marekani.
Jumatano iliyopita waasi wa M23 walitoa taarifa wakidai kuuteka mji wa kimkakati wa Uvira, ambao ni kitovu muhimu cha kibiashara karibu na mpaka wa nchi hiyo na Burundi.
Mji wa Uvira umekuwa ukitambuliwa kama makao makuu ya muda ya jimbo la Kivu Kusini tangu waasi wa M23 waidhibiti Bukabu mapema mwaka huu.