Zaidi ya watu 500,000 wamekimbia makazi yao katika wiki 2 za mapigano DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134326-zaidi_ya_watu_500_000_wamekimbia_makazi_yao_katika_wiki_2_za_mapigano_drc
Zaidi ya watu 500,000, wakiwemo zaidi ya watoto 100,000, wamekimbia makazi yao tangu Desemba 1 kutokana na mapigano makali katika mkoa wa Kivu Kusini wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Hayo yalitangazwa jana Jumapili na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).
(last modified 2025-12-15T03:25:10+00:00 )
Dec 15, 2025 03:25 UTC
  • Zaidi ya watu 500,000 wamekimbia makazi yao katika wiki 2 za mapigano DRC

Zaidi ya watu 500,000, wakiwemo zaidi ya watoto 100,000, wamekimbia makazi yao tangu Desemba 1 kutokana na mapigano makali katika mkoa wa Kivu Kusini wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Hayo yalitangazwa jana Jumapili na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).

Katika taarifa yake hiyo, UNICEF imesema kuwa "ina wasiwasi mkubwa" kutokana na kuongezeka kwa kasi mapigano huko Kivu Kusini na kuwalazimisha mamia ya maelfu ya watoto na familia zao kukimbilia maeneo mengine ya ndani ya DRC na wengine kuvuka mipaka na kuingia katika nchi jirani za Burundi na Rwanda.

UNICEF imetoa mwito kwa pande zote zinazopigana, kuheshimu usalama wa raia na sheria ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu.

Huku mapigano hayo yakizidi kuwa makubwa, idadi ya watu wanaokimbia maeneo yao nayo inazidi kuongezeka na kwamba mamia ya watu, wakiwemo watoto wadogo wanaendelea kuuawa tangu Desemba 2 huko Kivu Kusini.

Wananchi wa kawaida hasa wanawake na watoto ndio wahanga wakuu wa vita huko DRC

 

Wimbi kubwa na la ghafla la watu wanaokimbia mapigano limesajiliwa katika nchi jirani ya Burundi. Kati ya Desemba 6 na Desemba 11, zaidi ya wageni 50,000 walisajiliwa huku karibu nusu yao wakiwa ni watoto wadogo na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kama zinavyosema taarifa za UNICEF.

Mapema wiki hii, kundi la waasi la Harakati ya Machi 23 (M23) lilitangaza kwamba limeuteka mji wa Uvira, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa katika jimbo la Kivu Kusini karibu na mpaka wa Burundi. Mashambulizi yanaendelea kuripotiwa hadi hivi sasa kwenye mji huo na wimbi la wakimbizi linazidi kuwa kubwa.