Jeshi la Kongo laukomboa mji wa mashariki wa Uvira kutoka kwa waasi wa M23
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135694-jeshi_la_kongo_laukomboa_mji_wa_mashariki_wa_uvira_kutoka_kwa_waasi_wa_m23
Vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimeudhibiti tena mji wa mashariki wa Uvira baada ya waasi wa kundi la M23 kuondoka katika mji huo.
(last modified 2026-01-20T07:17:15+00:00 )
Jan 20, 2026 07:17 UTC
  • Jeshi la Kongo DR
    Jeshi la Kongo DR

Vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimeudhibiti tena mji wa mashariki wa Uvira baada ya waasi wa kundi la M23 kuondoka katika mji huo.

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetoa taarifa  na kuutuhumu Muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC) au Congo River Alliance; muungano wa waasi wa mashariki mwa nchi hiyo ambao unalijumuisha kundi la waasi M23, na wale  wanaodaiwa kuwa wanajeshi wa Rwanda, kwa kufanya "uporaji ulioratibiwa' katika mji wa Uvira kabla ya kuondoka katika mji huo. 

Jeshi la Kongo limesema kuwa takriban raia 20 waliohusika katika uporaji huko Uvira tayari wamekamatwa na  kwamba wana kesi ya kujibu. Jeshi la Kongo limetuma askari katikak mji wa Uvira na maeneo yanayouzunguka mji huo ili kuimarisha udhibiti na kulinda wakazi  wa mji huo na mali zao.

Jeshi la Kongo limeukomboa mji wa Uvira mwezi mmoja baada ya muungano wa Congo River Alliance na waasi wa M23 kuuteka mji huo Desemba 10 mwaka jana.

Mji wa Uvira ni kitovu muhimu cha kibiashara karibu na mpaka na Burundi ambao umekuwa ukitumika kama makao makuu ya muda ya jimbo la Kivu Kusini.

Waasi wa M23 walisonga mbele katika maeneo kadhaa ya jimbo la Kivu Kusini licha ya makubaliano ambayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitia saini mjini Washington kati yake na Rwanda  Desemba mwaka jana.