Afya ya kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Uganda aliyeko gerezani yadaiwa kuzorota
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135718-afya_ya_kiongozi_mkongwe_wa_upinzani_nchini_uganda_aliyeko_gerezani_yadaiwa_kuzorota
Chama cha upinzani nchini Uganda cha People’s Front for Freedom kimesema katika taarifa kwamba afya ya kiongozi mkongwe wa upinzani nchini humo Kizza Besigye “iko katika hali mbaya na inaendelea kudhoofika,” na kutoa mwito wa kutaka aruhusiwe kukaguliwa na madaktari wake binafsi pamoja na familia yake.
(last modified 2026-01-20T23:09:43+00:00 )
Jan 20, 2026 23:09 UTC
  • Afya ya kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Uganda aliyeko gerezani yadaiwa kuzorota

Chama cha upinzani nchini Uganda cha People’s Front for Freedom kimesema katika taarifa kwamba afya ya kiongozi mkongwe wa upinzani nchini humo Kizza Besigye “iko katika hali mbaya na inaendelea kudhoofika,” na kutoa mwito wa kutaka aruhusiwe kukaguliwa na madaktari wake binafsi pamoja na familia yake.

Hayo yanajiri baada ya Besigye, aliyeko gerezani kupelekwa katika kituo cha afya kilichopo katika mji mkuu, Kampala wakati usiku.

Besigye, mwanasiasa mkongwe ambaye alikuwa kiongozi maarufu zaidi wa upinzani nchini Uganda kabla ya kupanda kwa umaarufu wa Bobi Wine, anazuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali jijini Kampala. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ya uhaini, ambayo yeye mwenyewe anasema yanatokana na sababu za kisiasa.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba mtu aliyejitolea kwa ajili ya afya na uhuru wa wengine ananyimwa haki yake ya kupata matibabu,” ilieleza taarifa ya People’s Front for Freedom iliyotolewa jana Jumanne.

“Tunaitaka serikali na mamlaka za magereza kuwajibika kikamilifu kwa afya yake.”

Hata hivyo, Frank Baine, msemaji wa Idara ya magereza wa Uganda, amekanusha madai ya kudhoofika afya ya Besigye.

“Ilikuwa ni uangalizi wa kawaida tu,” amesema Baine alipozungumzia safari ya Besigye ya kupelekwa kwa daktari usiku na akaongezea kwa kusema: “asubuhi ya leo alikuwa akifanya mazoezi yake kama kawaida.”

Besigye aligombea urais mara ya mwisho mwaka 2016. Baadaye alisema, uchaguzi ni kupoteza muda katika nchi inayoongozwa na kiongozi wa kiimla ambaye mamlaka yake yanategemea majeshi ya usalama.

Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, alitangazwa siku ya Jumamosi kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Museveni alipata asilimia 71.6 ya kura huku mpinzani wake wa karibu zaidi, Bobi Wine, akipata asilimia 24.7.

Wine amekataa matokeo hayo akisema kuwa ni ya kighushi.../