OCHA: Watu laki tano wameathiriwa vibaya na mafuriko Msumbiji, mamba ni tishio mijini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135738-ocha_watu_laki_tano_wameathiriwa_vibaya_na_mafuriko_msumbiji_mamba_ni_tishio_mijini
Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA nchini Msumbiji amesema, mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha, yamesababisha majanga makubwa kwa maisha na mbinu za kujipatia kipato nchini humo, yakiongeza pia hatari ya mripuko wa magonjwa na kuyaweka maeneo ya mijini katika hatari ya kuzingirwa na mamba.
(last modified 2026-01-21T10:37:52+00:00 )
Jan 21, 2026 10:37 UTC
  • OCHA: Watu laki tano wameathiriwa vibaya na mafuriko Msumbiji, mamba ni tishio mijini

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA nchini Msumbiji amesema, mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha, yamesababisha majanga makubwa kwa maisha na mbinu za kujipatia kipato nchini humo, yakiongeza pia hatari ya mripuko wa magonjwa na kuyaweka maeneo ya mijini katika hatari ya kuzingirwa na mamba.

Paola Emerson, ameeleza hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwa njia ya intaneti na kuongeza kuwa majimbo ya Gaza, Sofala na Maputo ndiyo yaliyoathirika vibaya zaidi.

Akizungumza kutoka mji mkuu wa jimbo la Gaza, Xai Xai, Bi. Emerson amesema, zaidi ya watu nusu milioni wameathiriwa vibaya na mafuriko hayo, yaliyosababishwa na mvua kubwa katika wiki za mwanzo za mwaka mpya.

“Idadi inaendelea kuongezeka huku mafuriko makubwa yakiendelea na mabwawa yakiendelea kuachilia maji ili kuepuka kupasuka,” ameeleza afisa huyo wa UN na kuongezea kwa kusema: “asilimia 90 ya wananchi wa Msumbiji wanaishi katika nyumba zilizojengwa kwa matofali ya udongo, ambazo kimsingi huweza kumomonyoka baada ya siku chache za mvua”.

Kwa mujibu wa Bi. Emerson, vituo vya afya, barabara na miundombinu muhimu pia vimeathiriwa vibaya kwa kiasi kikubwa na kwamba karibu kilomita 5,000 za barabara zimeharibiwa katika majimbo tisa, ikiwemo barabara kuu inayounganisha mji mkuu wa Msumbiji, Maputo na maeneo mengine ya nchi, ambayo kwa sasa haipitiki, hali inayosababisha usumbufu mkubwa katika minyororo ya usambazaji.

Serikali ya Msumbiji imetangaza hali ya dharura ya kitaifa na imeanzisha kituo cha operesheni za dharura katika jimbo la Gaza.

Mji wa Xai-Xai, ulioko karibu na Mto Limpopo, umefurika, hali ambayo imesababisha uhamishaji wa wakazi.../