Sudan: Pendekezo lolote la kumaliza vita linapasa kulinda maslahi ya taifa na umoja wa ardhi ya nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136980-sudan_pendekezo_lolote_la_kumaliza_vita_linapasa_kulinda_maslahi_ya_taifa_na_umoja_wa_ardhi_ya_nchi_hiyo
Sudan imesema kuwa pendekezo lolote la kumaliza vita na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) linapasa kuzingatia maslahi makuu ya nchi hiyo, mshikamano na umoja wa ardhi nzima ya nchi hiyo.
(last modified 2026-05-10T14:24:40+00:00 )
Feb 24, 2026 04:30 UTC
  • Dagalo na al Burhan
    Dagalo na al Burhan

Sudan imesema kuwa pendekezo lolote la kumaliza vita na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) linapasa kuzingatia maslahi makuu ya nchi hiyo, mshikamano na umoja wa ardhi nzima ya nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema katika taarifa yake kuwa pendekezo au ubunifu wowote halimaanishi kuwa limekubaliwa au kuidhinishwa na serikali ya Sudan.”

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesisitiza kuwa: Mapendekezo yoyote ya kukomesha vita na kurejesha amani nchini humo yanapasa kuzingatia maslahi makuu ya nchi, usalama wa taifa wa Sudan, umoja wa ardhi yote ya  Sudan, mshikamano wa taasisi zake na mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesisitiza kuwa Sudan ni nchi huru na inachukua maamuzi na misimamo kwa mujibu wa maslahi yake ya kitaifa. 

Massad Boulos mshauri wa ngazi ya juu wa Marekani nchini Sudan awali alikuwa amependekeza mkakati wa nguzo tano ili kuhitimisha vita huko Sudan.

Boulos alisema katika hotuba yake katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Washington inashirikiana na pande nyingine washirika zikiwemo Misri, Saudi Arabia, Imarati na Uingereza kushinikiza kufikiwa mapatano ya kusitisha vita nchini Sudan bila ya masharti. 

Sudan imetumbukai katiak vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kuwania madaraka tangu Aprili 2023; vita ambavyo hadi sasa vimeuwa makumi ya maelfu ya Wasudani na kupelekea wengine wasiopungua milioni 13 kuwa wakimbizi.