Nigeria yataka msaada kukabiliana na mshtuko wa kiuchumi uliochochewa na vita dhidi ya Iran
Waziri wa Fedha wa Nigeria, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa muungano wa nchi zinazoendelea unaojulikana kama G24, amesema kwamba taasisi za kifedha za kimataifa zinapaswa kuongeza hatua za kusaidia mataifa yaliyo hatarini ili kuvuka mishtuko ya kiuchumi inayosababishwa na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Wale Edun alikuwa alizungumza katika mkutano wa kundi la G24 uliofanyika pembezoni mwa mkutano wa majira ya machipuko wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia mjini Washington. Amebainisha kuwa: “Tunatarajia taasisi hizi zitachukua hatua zaidi. Bila shaka tunahitaji taasisi hizi zisaidie kupunguza gharama kwa nchi zinazoendelea.”
Kundi la G24 lina jukumu la kuoanisha misimamo ya nchi zinazoendelea kuhusu masuala ya kifedha na maendeleo ya uchumi.
Waziri huyo amebainisha kuwa kutokana na kupungua kwa misaada ya maendeleo, misaada wa kimataifa, na kuongezeka kwa mzigo wa kulipa madeni, mtiririko halisi wa fedha kuelekea nchi zinazoendelea kwa sasa umekuwa hasi.
Kupanda kwa bei ya mafuta duniani kutokana na vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran kumesababisha bei ya petroli nchini Nigeria kuongezeka kwa takribani asilimia 65. Hata uzalishaji wa kiwango cha juu katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote, ambacho ni kikubwa zaidi Afrika Magharibi, haujafanikiwa kudhibiti athari za vita Asia Magharibi.
Katika mazingira haya, waziri wa fedha amesema Nigeria itaendelea kutafuta msaada thabiti zaidi wa kifedha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa. Kwa miaka mingi Nigeria ilihifadhi mfumo wa ruzuku ya mafuta uliogharimu kiwango kikubwa cha fedha, lakini serikali ya sasa imeufuta. Rais Bola Tinubu, mara tu baada ya kuingia madarakani katikati ya mwaka 2023, alianza kutekeleza mageuzi makubwa ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kufuta ruzuku ya petroli iliyokuwa ikimezwa na gharama kubwa.
Kundi la G24 liliundwa mwaka 1971 kama tawi la kundi la G77 kwa madhumuni ya kuoanisha misimamo ya nchi zinazoendelea katika masuala ya kifedha na maendeleo ya uchumi. Kwa sasa lina wanachama 28, na uenyekiti wake wa kipindi hiki uko mikononi mwa Nigeria.