Kenya yaongeza bei ya mafuta kufuatia vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i137852-kenya_yaongeza_bei_ya_mafuta_kufuatia_vita_vya_marekani_na_israel_dhidi_ya_iran
Serikali ya Kenya imepandisha bei za rejareja za bidhaa za mafuta kwa kiwango cha hadi asilimia 24.2, ikizingatia ongezeko la ghafla la bei ya mafuta ghafi duniani na changamoto za usambazaji wa nishati zinazosababishwa na vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Iran..
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 16, 2026 06:19 UTC
  • Meli za Mafuta katika Lango Bahari la Hormuz nchini Iran
    Meli za Mafuta katika Lango Bahari la Hormuz nchini Iran

Serikali ya Kenya imepandisha bei za rejareja za bidhaa za mafuta kwa kiwango cha hadi asilimia 24.2, ikizingatia ongezeko la ghafla la bei ya mafuta ghafi duniani na changamoto za usambazaji wa nishati zinazosababishwa na vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Iran..

Taarifa hiyo imetolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Mafuta Kenya (EPRA).

Kwa mujibu wa EPRA, bei ya petroli kwa lita moja imeongezeka kwa asilimia 16.1 na kufikia shilingi 206.97 za Kenya (sawa na dola 1.60 za Marekani). Bei ya dizeli imepanda kwa asilimia 24.2 hadi shilingi 206.84, huku mafuta ya taa yakisalia kwenye shilingi 152.78 kwa lita.

EPRA imeeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa gharama za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, ambazo zimepanda kwa takribani asilimia 68.7, hivyo kuathiri moja kwa moja bei za rejareja.

Mwezi Machi, mamlaka hiyo haikubadili bei za mafuta, ikitaja kuwa athari za mivutano ya kijeshi katika ukanda wa Asia Magharibi bado hazikuwa zimeonekana moja kwa moja katika soko la ndani.

Kenya hununua karibu mafuta yake yote kutoka eneo la Asia Magharibi kupitia makubaliano ya serikali kwa serikali na kampuni za Ghuba ya Uajemi, ikiwemo Aramco ya Saudi Arabia, ADNOC ya Abu Dhabi na Shirika la Kitaifa la Mafuta la Imarati.

Masaa machache kabla ya bei mpya kuanza kutumika Jumanne usiku, madereva jijini Nairobi walifurika vituo vya mafuta wakiharakisha kujaza magari yao, hali iliyosababisha foleni ndefu.

Aidha, EPRA imetangaza kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa kutoka asilimia 16 hadi 13, ikisema hatua hiyo inalenga kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi kutokana na kupanda kwa bei katika soko la kimataifa. Ongezeko hilo la bei za petroli na dizeli nchini Kenya linatazamiwa kuibua mfumuko mkubwa wa bei na hivyo kuwaathiri Wakenya katika miezi ijayo.

Baada ya kushambuliwa katika vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Marekani ikishirikiana na Israel, Iran sasa imechukua udhibiti eneo la Lango Bahari la Hormuz ambayo ni njia kuu ta asilimia 20 ya mafuta ya dunia hasa Yale ambayo hutumika Afrika Mashariki.