Afrika yaweka rekodi, yatuma timu 10 katika Kombe la Dunia huku mashindano ya 2026 yakianza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139064-afrika_yaweka_rekodi_yatuma_timu_10_katika_kombe_la_dunia_huku_mashindano_ya_2026_yakianza
Afrika inaandika historia katika Kombe la Dunia FIFA 2026 kwa kuwakilishwa na timu 10, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kufikiwa na bara hilo katika mashindano hayo.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jun 11, 2026 11:15 UTC
  • Afrika yaweka rekodi, yatuma timu 10 katika Kombe la Dunia huku mashindano ya 2026 yakianza

Afrika inaandika historia katika Kombe la Dunia FIFA 2026 kwa kuwakilishwa na timu 10, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kufikiwa na bara hilo katika mashindano hayo.

Mashindano hayo yanaanza Alhamisi nchini Mexico, ambapo Afrika Kusini itakutana na wenyeji wenza Mexico katika mechi ya ufunguzi. Kwa mara ya kwanza, Afrika ina uwakilishi wa timu za tarakimu mbili katika jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.

Timu zitakazopeperusha bendera ya bara hilo katika mashindano yaliyopanuliwa hadi timu 48 nchini Canada, Mexico na Marekani ni: Algeria, Cape Verde, Côte d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ghana, Morocco, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia.

Huu ni wakati wa kihistoria kwa soka la Afrika, miaka minne baada ya Morocco kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia katika Qatar 2022.

Kuongezeka uwakilishi wa Afrika kwenye Kombe la Dunia kunalipa bara hilo fursa pana zaidi ya kujenga juu ya mafanikio hayo na kusonga mbele zaidi katika mashindano kuliko ilivyowahi kushuhudiwa hapo awali.

Sasa Afrika ina fursa nyingine ya kuonyesha kwamba nafasi yake katika Kombe la Dunia haikui kwa idadi pekee, bali pia kwa kiwango cha matarajio na azma.

Hata hivyo, ushiriki wa Afrika umekumbwa na utata baada ya mwamuzi wa Kisomali, Omar Abdulkadir Artan, kukosa fursa ya kuchezesha katika Kombe hili la Dunia baada ya Marekani kumzuia kuingia nchini humo.

Artan, ambaye ni miongoni mwa waamuzi bora wa Afrika na yumo katika orodha ya waamuzi 52 wa Kombe la Dunia ya FIFA, “alizuiwa kuingia Marekani kutokana na masuala ya uhakiki wa kiusalama.” Rais Trump wa Marekani amekuwa akitoa matamshi ya kibaguzi na chuki dhidi ya Somalia na Wasomali na hiyo imetajwa kuwa sababu kuu ya kuzuiwa refa hiyo maarufu barani Afrika

Marekani pia imekabiliwa na lawama kwa kuidhalilisha timu za soka ya Senegal katika ukaguzi wa kiusalama wakati timu hiyo ilipowasilia katika uwanja wa ndege.

Zaidi ya robo ya nchi zinazoshiriki katika Kombe la Dunia, nyingi zikiwa ni za Afrika, zinaathiriwa na vizuizi vya kusafiri  na pia zinakabiliwa na viwango vya juu vya kukataliwa kwa visa za maafisa na mashabiki.

Aidha Kutokana na changamoto za visa na mvutano wa kisiasa unaoendelea, timu ya taifa ya Iran imelazimika kuweka kambi nchini Mexico.

Mechi zote tatu za Iran katika hatua ya makundi zitachezwa nchini Marekani, lakini kwa hali isiyo ya kawaida, wachezaji na maafisa wa timu hiyo watalazimika kuingia na kutoka nchini humo siku hiyohiyo ya kila mechi kutokana na vizuizui vilivyowekwa na utawala wa Trump.