Interpol: Akili Mnemba (AI) inatumika katika 55% ya uhalifu wa mtandaoni barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140444-interpol_akili_mnemba_(ai)_inatumika_katika_55_ya_uhalifu_wa_mtandaoni_barani_afrika
Ripoti ya karibuni ya Polisi ya Kimataifa, Interpol, kuhusu tishio la uhalifu wa mtandaoni barani Afrika kwa mwaka 2026 imetoa onyo kali kuhusu jinsi teknolojia ya Akili Mnemba (AI) inavyotumiwa kudhoofisha usalama wa kiuchumi na kijamii katika mataifa bara hilo.
(last modified 2026-08-06T03:48:10+00:00 )
Aug 06, 2026 03:43 UTC
  • Interpol: AI inatumiwa katika uhalifu Afrika.
    Interpol: AI inatumiwa katika uhalifu Afrika.

Ripoti ya karibuni ya Polisi ya Kimataifa, Interpol, kuhusu tishio la uhalifu wa mtandaoni barani Afrika kwa mwaka 2026 imetoa onyo kali kuhusu jinsi teknolojia ya Akili Mnemba (AI) inavyotumiwa kudhoofisha usalama wa kiuchumi na kijamii katika mataifa bara hilo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, AI inatajwa kuhusika katika 55% ya uhalifu wote wa mtandaoni ulioripotiwa. Teknolojia hiyo imewapa wahalifu uwezo wa kutekeleza mashambulizi kwa kasi kubwa, kwa kiwango kikubwa zaidi, na kwa mbinu ambazo ni vigumu kuzitambua. Takwimu kutoka nchi 36 za Kiafrika zinaonyesha kuwa hasara ya kifedha inayotokana na uhalifu huo imeongezeka mara mbili tangu mwaka 2024, ikipanda kutoka dola milioni 192 hadi kufikia dola milioni 484.

Uhalifu wa njia ya mtandao (online fraud) umebainika kuwa ndio tishio kubwa zaidi barani, huku wahalifu wakitumia majukwaa ya fedha za simu, mitandao ya kijamii na AI kufikia idadi kubwa ya watu. Ripoti hiyo inabainisha mgawanyo wa kikanda wa uhalifu huo ambapo Afrika Mashariki imegeuka kuwa kitovu cha ulaghai unaolenga mifumo ya malipo ya simu na mashambulizi ya kusaka fidia (ransomware). Eneo la Afrika Magharibi na Kati ndipo penye mkusanyiko mkubwa wa utapeli wa barua pepe za kibiashara (BEC) na ulaghai wa mapenzi mtandaoni. Eneo la kusini mwa Afrika limeibuka kama shabaha kuu ya magenge ya kimataifa ya uhalifu wa mtandaoni kutokana na kiwango chake cha juu cha muunganisho wa kidijitali.

Aidha, ripoti imeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu maudhui ghushi ya teknolojia za mtandaoni (deepfakes) ambayo yamekuwa yakitumika vibaya katika matukio ya vitisho vya kidijitali na unyanyasaji wa mtandaoni. Hili ni tishio kwa maadili na heshima ya jamii, ambalo linahitaji hatua madhubuti za kisheria na ulinzi wa maadili ya umma.

Ingawa mataifa kama Senegal yamechukua hatua za kuanzisha mifumo ya kuripoti uhalifu wa mtandaoni, na nchi 17 zimeimarisha sheria zao katika uwanja huo, lakini bado kuna haja ya dharura. Interpol imeweka wazi kuwa zaidi ya washukiwa 1,500 wamekamatwa katika operesheni za kimataifa, huku zaidi ya dola milioni 100 za mapato haramu zikitaifishwa.