Afrika Kusini yaadhimisha Maandamano ya Wanawake ya 1956 – mapambano ya uhuru bado yanaendelea
-
Afrika Kusini yaadhimisha Maandamano ya Wanawake ya 1956 – mapambano ya uhuru bado yanaendelea
Afrika Kusini, leo Jumapili, inaadhimisha miaka 70 tangu Maandamano ya Wanawake ya 1956, wakati wanawake wapatao 20,000 wa mbari na rangi zote walipoandamana hadi mji mkuu wa utawala, Pretoria, kupinga sheria za ubaguzi wa rangi zilizowalazimisha wanawake weusi kubeba vibali vilivyowazuia kutembea.
Maandamano hayo yalikuwa hatua muhimu sana katika mapambano dhidi ya utawala wa wazungu wachache.
Lakini miongo saba baada ya kujiweka katika hatari ya kukamatwa, kuteswa na hata kuuawa ili kupinga sheria za ubaguzi wa rangi, wanawake wengi wa Afrika Kusini wanasema mapambano yao ya uhuru nchini Afrika Kusini hayajakamilika na kwamba wanaendelea kukabiliana na viwango vya juu vya ukatili wa kijinsia, umaskini na ukosefu wa usawa.
Utafiti uliofadhiliwa na United Nations Women mwaka 2024 uligundua kuwa zaidi ya mwanamke mmoja kati ya watatu wa Afrika Kusini wamepitia ukatili wa kimwili au kingono katika maisha yao.
Ramnie Dinat, mwenye umri wa miaka 84, alikuwa kijana wakati wa maandamano ya Agosti 9, 1956. Anakumbuka akimsaidia mama yake, Ama Naidoo, mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi, kuandaa wanawake kabla ya maandamano hayo. Wanawake weusi, wanawake wa asili ya India kama Naidoo, na hata baadhi ya wanawake weupe walishirikii katika maandamano siku hiyo.
"Kila mtu alipaswa kuwa na nafasi katika tukio hilo. Haikuwa rahisi kuandaa tukio hilo. Ilibidi uende mlango hadi mlango, upige hodi na kuwaambia wanawake watoke nje kwenye maandamano," Dinat ameambia The Associated Press.
Viongozi na washiriki wengi wa maandamano hayo baadaye walifungwa katika Gereza la Wanawake, ambapo wanaharakati walitenganishwa kulingana na rangi zao, kama ulivyokuwa ukifanya utawala wa ubaguzi wa rangi kila mahali nchinii Afrika Kusini.
Nolubabalo Memese, Meneja wa Huduma za Wageni katika Constitution Hill anasema kwamba gereza hilo lilibuniwa ili kuvunja, kudhalilisha na kudunisha ubinadamu.
Ameongeza kuwa wanawake weusi waliofungwa gerezani hawakuruhusiwa kuvaa nguo za ndani au kuwa na taulo za usafi zinazofaa.
Umoja wa Mataifa umeelezea viwango vya juu vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana nchini Afrika Kusini kuwa ni mgogoro na "jeraha la kitaifa."
Takwimu za serikali zinasema wanawake ndio wanaosumbuliwa zaidi na ukosefu wa ajira kuliko wanaume, kufanya kazi ya utunzaji bila malipo na bado wana uwakilishi mdogo katika uongozi mkuu nchini Afrika Kusini.