Shirika la Taifa la Mafuta la Libya lasema halitaweza kutekeleza mikataba katika kituo cha Zawiya baada ya hujuma ya droni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140586-shirika_la_taifa_la_mafuta_la_libya_lasema_halitaweza_kutekeleza_mikataba_katika_kituo_cha_zawiya_baada_ya_hujuma_ya_droni
Shirika la Taifa la Mafuta la Libya leo Jumanne limetangaza kuwa halitaweza kutekeleza mikataba na kwamba litasimamisha kikamilifu utendaji katika eneo la mafuta la Zawiya, magharibi mwa Libya, kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani kwenye vituo vyake.
(last modified 2026-08-11T11:22:47+00:00 )
Aug 11, 2026 11:20 UTC
  • Kituo cha mafuta cha Zawiya, Libya chashambuliwa
    Kituo cha mafuta cha Zawiya, Libya chashambuliwa

Shirika la Taifa la Mafuta la Libya leo Jumanne limetangaza kuwa halitaweza kutekeleza mikataba na kwamba litasimamisha kikamilifu utendaji katika eneo la mafuta la Zawiya, magharibi mwa Libya, kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani kwenye vituo vyake.

Indhari hii imetolewa saa chache baada ya shirika hilo linalomilikiwa na serikali kutangaza hali ya dharura ya kiwango cha juu katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Zawiya baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani kuchomoa tanki la kuhifadhia mafuta lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 4.5 za petroli.

Vituo vya mafuta katika mji wa Zawiya, takriban kilomita 40 (maili 25) magharibi mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli, vimeshambuliwa mara kwa mara katika siku za hivi karibuni kufuatia mapigano kati ya makundi yenye silaha katika eneo hilo.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu, Shirika la Taifa la Mafuta la Libya lilieleza kuwa mitambo ya mafuta huko Zawiya "inaendelea kushambuliwa kwa hujuma zinazofanywa na ndege zisizo na rubani zinazoendeshwa kutokea mbali."

Shirika hilo limesema kuwa timu za kuzima moto na za usalama kutoka kiwanda cha kusafisha mafuta cha Zawiya, Brega na kampuni jirani za mafuta hadi jana zilikuwa zikiendelea na juhudi za kudhibiti moto katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Zawiya.

Wiki iliyopita, mapigano kati ya makundi yenye silaha mjini Zawiya yalienea hadi katika mji wa karibu wa Surman, na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa na kupelekea wafungwa kutoroka gerezani.