Mtawala wa Dubai 'azongwa' kwenye mitaa ya London kwa kuhusika UAE katika vita vya Sudan
-
Mohammed bin Rashid Al-Maktoum
Mtawala wa Dubai ambaye ni waziri mkuu wa Muungano wa Falme za Kiarabu, UAE amezongwa kwa maneno katika mitaa ya katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London kuhusiana na ushiriki wa nchi yake katika vita vya ndani nchini Sudan.
Video iliyosambaa mitandaoni imemuonyesha mwanamume mmoja Msudan akimrushia maneno Mohammed bin Rashid Al-Maktoum na msafara wake walipokuwa wanatembea katika eneo la matajiri la Knightsbridge.
“Waimarati na UAE, wanawaua watu wa Sudan,” alipaza sauti mwanamume huyo kutokea ng'ambo ya barabara akimhutubu mtawala wa Dubai na kundi alilokuwa ameandamana nalo na kuongezea kwa kusema: “UAE inaua watu katika nchi yangu. Acheni kuwaua watu wangu.”
Katika mazingira hayo, mwanamume mmoja, anayeonyesha kuwa ni Muimarati aliyemo kwenye msafara wa al-Maktoum, anaonekana akitoa maneno machafu ya matusi na ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Msudan huyo kwa kumwambia: "kwenda zako, kwenda zako wewe na hao watu wako… kwenda zako mwanaharamu mweusi".
"Umesema mweusi?", anasikika Msudan huyo akihoji, huku Muimarati huyo akimjibu tena kwa maneno ya matusi na kumfuata mtu huyo upande wa pili wa barabara kukabiliana naye.
"Acheni kuwaua Wasudan," aliendelea kusema Msudan huyo. "Imarati na UAE wanawaua watu wa Sudan. Wanawaua watu katika nchi yangu ... Mohammed bin Zayed, wanawaua watu katika nchi yangu," alisema, akimaanisha rais wa Muungano wa Falme za Kiarabu.
Japokuwa Imarati inaendelea kukanusha, lakini sasa kuna ushahidi mwingi unaotilia nguvu dai kwamba nchi hiyo ndogo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi inaunga mkono Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vya Sudan RSF, ambavyo vimeshutumiwa na Umoja wa Mataifa kwa kufanya mauaji ya kimbari wakati wa vita vya ndani nchini Sudan.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa, makundi ya kutetea haki za binadamu na ripoti za vyombo vya habari zimethibitisha kufanyika usafirishaji wa silaha ilizopelekewa RSF kupitia mitandao yenye makao yake Libya, Chad na eneo la Somalia lililojitenga la Somaliland…/