Uturuki yaitaka Tunisia imuachie kiongozi wa chama cha Kiislamu cha Ennahda anayesota gerezani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140674-uturuki_yaitaka_tunisia_imuachie_kiongozi_wa_chama_cha_kiislamu_cha_ennahda_anayesota_gerezani
Spika wa Bunge la Uturuki, Numan Kurtulmus, ametoa wito wa kutaka kiongozi wa chama cha Kiislamu cha Ennahda na Spika wa zamani wa Bunge la Tunisia, Rached Ghannouchi, ambaye anaendelea kusota gerezani, apatiwe matibabu na kuachiwa kwa kuzingatiwa utu na ubinadamu.
(last modified 2026-08-15T03:53:00+00:00 )
Aug 15, 2026 03:51 UTC
  • Uturuki yaitaka Tunisia imuachie kiongozi wa chama cha Kiislamu cha Ennahda anayesota gerezani

Spika wa Bunge la Uturuki, Numan Kurtulmus, ametoa wito wa kutaka kiongozi wa chama cha Kiislamu cha Ennahda na Spika wa zamani wa Bunge la Tunisia, Rached Ghannouchi, ambaye anaendelea kusota gerezani, apatiwe matibabu na kuachiwa kwa kuzingatiwa utu na ubinadamu.

Kurtulmus amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Uturuki NSosyal, kwamba anafuatilia kwa karibu hali ya Ghannouchi, ambaye amemtaja kuwa “miongoni mwa watu mashuhuri katika mapambano ya amani, demokrasia na mshikamano.”

Ameongeza kuwa, Ghannouchi amesitisha kugoma kula na kususia dawa, baada ya kuombwa kufanya hivyo na madaktari wanaofuatilia hali yake.

“Kwa kuzingatia umri wake mkubwa na matatizo ya kiafya aliyonayo, uzito wa hali ya Ghannouchi haupaswi kupuuzwa,” ameeleza spika huyo wa bunge la Uturuki.

Kurtulmus amemtaja Ghannouchi kuwa mtu aliyejitolea maisha yake kwa “mustakabali wa watu wa Tunisia, uhuru, haki na demokrasia,” akisema licha ya mashinikizo, kuishi uhamishoni na kufungwa, hakuachana na “maadili aliyoyaamini na mapambano yake ya kidemokrasia.”

Spika wa bunge la Uturuki amesema, Ghannouchi amepata kutambuliwa kwa kiwango kikubwa nchini Tunisia na kimataifa kutokana na “msimamo wake wa kidemokrasia wakati wa kipindi cha mpito, msingi wake imara wa kielimu na mawazo yake”, na akaongezea kwa kusema: “kwa kuakisi uhusiano wa kina wa kindugu uliopo kati ya watu wa Uturuki na Tunisia, namuombea afya njema na natumaini kwamba atarejea katika hali nzuri ya kiafya haraka iwezekanavyo,”

Aidha, amesema: “jambo tunalolitamani zaidi ni kwamba apewe kikamilifu msaada wa matibabu unaohitajika, apewe mazingira ya haki na ya kibinadamu yanayohitajika kwa ajili ya kuheshimu utu wa binadamu, na aachiliwe.”

Ghannouchi, ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tunisia lililovunjwa na Rais Kais Saied, amekuwa gerezani tangu alipokamatwa Aprili 17, 2023.

Mahakama iliamuru azuiliwe katika kesi iliyohusiana na matamshi yaliyodaiwa kutolewa na yeye, akishtakiwa kwa “kufanya uchochezi dhidi ya usalama wa taifa.” Baadaye alihukumiwa kifungo jela katika kesi kadhaa, lakini ameyakana mashtaka hayo akisema, yametokana na matashi ya kisiasa…/