UN: Kikomboleo cha dola milioni 50 kilichochea mashambulizi ya Al-Qaeda nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140696-un_kikomboleo_cha_dola_milioni_50_kilichochea_mashambulizi_ya_al_qaeda_nchini_mali
Umoja wa Mataifa umearifu kuwa fedha za kikomboleo takriban dola milioni 50, zilizolipwa mwishoni mwa mwaka 2025 ili kuwaachia huru mateka nchini Mali, zilisaidia kufadhili wanamgambo wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi Al-Qaeda na hujuma zao katika eneo zima la magharibi mwa Afrika.
(last modified 2026-08-16T03:12:19+00:00 )
Aug 16, 2026 03:07 UTC
  • Wapiganaji wa al Qaeda
    Wapiganaji wa al Qaeda

Umoja wa Mataifa umearifu kuwa fedha za kikomboleo takriban dola milioni 50, zilizolipwa mwishoni mwa mwaka 2025 ili kuwaachia huru mateka nchini Mali, zilisaidia kufadhili wanamgambo wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi Al-Qaeda na hujuma zao katika eneo zima la magharibi mwa Afrika.

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo iligawanywa upya kwa wanamgambo wenye silaha katika eneo la Sahel, huku sehemu nyingine ikipelekwa kwa tawi la Al-Qaeda katika Rasi ya Uarabuni na kwa uongozi mkuu wa kundi hilo.

Ripoti hiyo haimtaji mateka wala kuthibitisha ni nani aliyefanya malipo hayo ingawa vyanzo vya kikanda vinasema kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ndio uliolipa fedha hizo za kuwakomboa mateka.

Vyanzo hivyo vya habari vimeeleza kuwa raia wa Imarati (UAE), pamoja na mateka wengine wawili wa kigeni waliachiliwa huru katika makubaliano hayo. UAE haikutoa maoni kuhusu tukio hilo, lakini ilisema inaendelea kuchukua hatua dhidi ya misimamo mikali na vitendo vya ugaidi.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa vitendo vya kuwateka nyara watu vimekuwa vikitumiwa kama chanzo cha kujipatia fedha na ni njia inayotumiwa na wanamgambo kudhoofisha imani ya wananchi kwa serikali.

Muungano wa wanamgambo wanaobeba silaha kwa jina JNIM, wenye makao yake nchini Mali hivi sasa una wapiganaji kati ya 7,000 na 8,000 katika eneo lote la Sahel, huku nusu yao wakiwa nchini Mali.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa fedha za kikombolea zinayasaidia makundi hayo ya uhalifu kununua silaha, kugharamia shughuli za uendeshaji na kupanua wigo wa uasi wao katika eneo la Sahel barani Afrika.