Mkuu wa Baraza la Uongozi Sudan: Jeshi liko tayari kwa amani; apinga kurejea madarakani RSF
-
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa Baraza la Uongozi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, amesema kuwa jeshi bado limedhamiria kuwashinda wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF)—kikosi cha kijeshi kisicho rasmi- na amesisitiza kuwa jeshi liko tayari kupokea kile alichokiita juhudi za "kweli" za amani.
Katika hotuba yake ya kuadhimisha miaka 72 tangu kuanzishwa Jeshi la Sudan, Jenerali al Burhan ameeleza kuwa azma ya jeshi hilo ya kupambana na kulishinda kundi la RSF "haimaanishi kupuuza mpango wowote wa kweli wa kurejesha amani.
"Juhudi zetu katika suala hili hazijasimama tangu miezi ya awali ya uasi, lakini hatutakubali amani ambayo haijakamilika, au amani itakayowarejesha mamlakani wahalifu na wauaji—yaani wanamgambo wa Dagalo na wafuasi wake," amesema Mkuu wa Baraza la Uongozi la Sudan.
"Msimamo wetu uko wazi tangu Mei 2023: Njia ya kuelekea amani inaaanzia kwa wanamgambo hawa kuweka chini silaha zao na kukusanyika katika maeneo yaliyotengwa, raia kurejea katika maeneo yao na maisha kurejea katika hali ya kawaida, kupewa huduma, usalama, ulinzi na ufuatiliaji. Baada ya hapo, hali ya wanamgambo ambao si watenda jinai inaweza kuzingatiwa," ameongeza Jenerali Abdel Fattah al Burhan.
Katika nyanja ya kisiasa, Jenerali al Burhan amesema kuwa ameanzisha mazungumzo na makundi ya kitaifa ambayo "yanaunga mkono dola ya Sudan na kusimamia umoja na taasisi zake," kwa lengo la kuwashirikisha katika kukamilisha uundaji wa taasisi za dola, likiwemo baraza la kutunga sheria.