UN: Ebola inaua mtu mmoja kila baada ya nusu saa huko Congo DR
-
Jeneza la muathiriwa wa Ebola, Congo DR.
Tom Fletcher, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu, ametangaza kwamba mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo sasa unaua mtu mmoja kila baada ya nusu saa, akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kupambana na mlipuko huo.
Fletcher amesema katika taarifa kwamba mlipuko huu ndio "msambao wa kasi zaidi kuwahi kutokea," akisisitiza haja ya kuharakisha na kupanua mwitikio na mshikamano wa kimataifa kabla hali haijabadilika na kuwa mbaya zaidi.
Baada ya kupitia juhudi za hivi karibuni za kudhibiti virusi hivyo, ambavyo huambukizwa kupitia kugusana na majimaji ya mwili na kusababisha homa ya kutokwa na damu, Fletcher ameonya kwamba "Ebola inashinda katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na hatuwezi kuruhusu virusi hivyo kuzidi mwitikio wetu."
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amefichua kwamba janga hilo sasa linaua mtu mmoja kila baada ya dakika 30, akieleza kuwa "idadi kubwa zaidi ya watu iko hatarini."
Fletcher pia amesisitiza haja ya kuongezwa mara mbili idadi ya sasa ya timu za kukabiliana na Ebola huko Congo ili kuhakikisha mazishi salama na yenye heshima, kuongeza mara mbili uwezo wa matibabu, kuboresha ufuatiliaji wa waliogusana na wagonjwa, na kupeleka mameneja wenye uzoefu zaidi.
Tangu mlipuko wa wa sasa utangazwe katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mnamo Mei 15, virusi vya Ebola vimewaua watu wasiopungua 2,128 kati ya zaidi ya 4,500 walioambukizwa. Umoja wa Mataifa hapo awali ulikuwa umeonya kuhusu hatari ya mlipuko huo ukisema ndio mbaya zaidi katika historia ya ugonjwa huo.
Inafaa kuelewa kwamba virusi vya kwanza vya Ebola viligunduliwa mwaka wa 1976 karibu na Mto Ebola nchini Congo DR, na mlipuko wa sasa ni wa 17 na mkubwa zaidi ambao nchi hiyo ya Afrika ya Kati imekabiliana nao.