Waziri Mkuu wa Sudan: Mazungumzo ya ndani kwa ajili ya maridhiano kuanza hivi karibuni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140738-waziri_mkuu_wa_sudan_mazungumzo_ya_ndani_kwa_ajili_ya_maridhiano_kuanza_hivi_karibuni
Waziri Mkuu wa Sudan, Kamil Idris ametangaza kuwa, mazungumzo ya ndani kati ya makundi mbalimbali ya Wasudan yataanza hivi karibuni, kwa lengo la kufikia maridhiano ya kina nchini humo na hatimaye kufanyika uchaguzi huru na wa haki.
(last modified 2026-08-17T09:56:51+00:00 )
Aug 17, 2026 09:55 UTC
  • Kamil Idris, Waziri Mkuu wa Sudan
    Kamil Idris, Waziri Mkuu wa Sudan

Waziri Mkuu wa Sudan, Kamil Idris ametangaza kuwa, mazungumzo ya ndani kati ya makundi mbalimbali ya Wasudan yataanza hivi karibuni, kwa lengo la kufikia maridhiano ya kina nchini humo na hatimaye kufanyika uchaguzi huru na wa haki.

Kamil Idris amesema hayo alipokutana na ujumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, ulioongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mohamed Khaled wa Algeria.

Waziri Mkuu huyo amesema, mchakato huo utalenga kufanikisha mageuzi ya kitaifa, maridhiano ya kina na marekebisho ya Katiba, na hatimaye kukamilishwa uchaguzi huru na wa haki ambapo wananchi wa Sudan watachagua uongozi mpya wa nchi.

Kamil Idris ameongeza kuuwa, mazungumzo hayo yatakuwa mchakato unaoongozwa na wananchi wote wa Sudan, akisisitiza kuwa, Wasudan wenyewe ndio wenye haki ya kuamua namna nchi yao itakavyoendeshwa.

Aidha, Waziri Mkuu huyo amesisitiza kuwepo kwa kile alichokiita “mistari myekundu isiyoweza kuvukwa,” ikiwa ni pamoja na kukataa kuwekwa katika kiwango kimoja Jeshi la Sudan na wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF, pamoja na kupinga uingiliaji wa mataifa ya kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan.

Sudan imekuwa katika vita tangu mwaka 2023, baada ya kuzuka kwa mzozo wa madaraka kati ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa Jeshi la Sudan, na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu kama Hemedti, ambaye anaongoza Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Mzozo huo umechochea ukosefu wa usalama nchini Sudan na kusababisha ongezeko kubwa la idadi ya wakimbizi na watu waliolazimika kuyahama makazi yao.