Rais wa Zambia aongoza katika matokeo ya awali huku upinzani ukidai kuchezewa rafu
-
Zoezi la kuhesabu kura nchini Zambia linaendelea huku Rais Hichilema akitarajiwa kutetea kiti chake cha urais
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, anaongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, hali inayomuweka katika nafasi nzuri ya kushinda muhula mwingine wa urais bila kufanyika duru ya pili.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia, baada ya zaidi ya nusu ya kura za majimbo ya uchaguzi kuhesabiwa, Hichilema alikuwa amepata karibu asilimia 59 ya kura.
Uchaguzi huo umefanyika huku ukigubikwa na madai kutoka upande wa upinzani kwamba watu wenye silaha walivamia makazi ya mpinzani mkuu wa Hichilema.
Hichilema anawania muhula wa pili kupitia Chama cha United Party for National Development, UPND. Ili kushinda katika duru ya kwanza, mgombea wa urais anatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Wakati huo huo, awali zoezi la kuhesabu kura lilisitishwa kutokana na ripoti za vurugu dhidi ya maafisa wa uchaguzi na kuibwa baadhi ya karatasi za kura, kabla ya kuanza tena baada ya tume kusema hali ya usalama imedhibitiwa.
Mpinzani wake wa karibu, Brian Mundubile wa chama cha upinzani cha National Reconciliation Party for Unity and Prosperity (NRPUP), alikuwa akifuatia akiwa amepata takribani theluthi moja ya kura. Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa ndani ya siku chache.
Hata hivyo, uongozaji wa Rais Hakainde Hichilema katika matokeo ya awali umefunikwa na ukosoaji wa waangalizi wa kimataifa, ambao tayari wameutaja mchakato wa kampeni kuwa usio wa haki, huku zoezi la kuhesabu kura likikumbwa na changamoto.
Zoezi la kuhesabu kura lilisimamishwa kwa takribani saa sita siku ya Ijumaa, baada ya kuripotiwa vitendo vya vurugu dhidi ya wafanyakazi wa vituo vya kupigia kura pamoja na madai ya kuibwa karatasi za kura zilizokuwa tayari zimewekewa alama.