UN yaonya: Mlipuko wa Ebola nchini DR Congo 'unaongezeka kwa kasi' baada ya zaidi ya watu 2,500 kuaga dunia
-
UN: Ebola inasambaa kwa kasi Congo DR.
Umoja wa Mataifa ulitangaza jana Ijumaa kwamba virusi vya Ebola vinaenea kwa kasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kuua zaidi ya watu 2,500, ukitoa wito wa kutolewa misaada zaidi na kuonya kwamba ufadhili uliotolewa hadi sasa utaisha ndani ya wiki chache.
Julian Harneis, mratibu mkuu wa Ebola wa Umoja wa Mataifa, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kutoka Bunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwamba virusi hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,500 katika nchi hiyo na vinaendelea kuenea kwa kasi.
Harneis amesema idadi ya vifo inaongezeka kila siku, na kwamba nusu ya vifo hivyo vilirekodiwa katika siku ishirini zilizopita.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameendelea kusema: "Kuenea kwa Ebola kumezidi uwezo wa juhudi zetu za kupambana nayo. Kunaongezeka na kupanuka kwa kasi zaidi kuliko juhudi zinazofanywa katika eneo lote ambalo limechoshwa na mzozo wa miongo mitatu, na hivyo kuzidisha mahitaji ya kibinadamu."
Mratibu mkuu wa Ebola wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba nidhamu ya umma iko hatarini, na kwamba huduma za msingi hasa huduma za afya, zimegawanyika, akieleza kwamba uingiliaji kati umekuwa mgumu sana, na kwamba idadi kubwa ya vikundi vyenye silaha vinafanya harakati katika maeneo yaliyoathiriwa na virusi hivyo, jambo linalotatiza utoaji wa huduma za matatibabu kwa watu.
Harness pia amesema kuwa wafanyakazi 43 wa huduma za afya wamefariki dunia kati ya 160 walioambukizwa virusi hivyo, huku wengine wakilengwa katika mashambulizi dhidi ya magari ya wagonjwa au vituo vya afya yanayofanywa na raia wenye hasira na waliofadhaishwa na mlipuko wa Ebola.
Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani, WHO, na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Africa CDC, zimekaribisha uamuzi wa kuipatia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, dozi 70,000 za chanjo ya Ervebo ili kuimarisha mapambano dhidi ya mlipuko wa Ebola aina ya Bundibugyo.
Kwa sasa, chanjo ya Ervebo imeidhinishwa kutumika dhidi ya Ebola aina ya Zaire. Ingawa tafiti za awali kwenye maabara na wanyama zinaonesha kuwa huenda ikatoa kinga dhidi ya aina ya Bundibugyo, ufanisi wake kwa binadamu bado haujathibitishwa.