UNICEF: Mgogoro wa njaa kwa watoto Somalia wazidi kuwa mbaya baada ya kupunguzwa misaada
-
Somalia na tatizo la njaa
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeonya kuwa, utapiamlo unaotishia maisha miongoni mwa watoto nchini Somalia unaongezeka kwa kasi, huku zaidi ya vituo 200 vya afya na lishe vikilazimika kufungwa kutokana na kupunguzwa misaada ya kimataifa.
Taarifa ya UNICEF imeeleza kuwa, nchi hiyo ya Pembe ya Afrika imeshuhudia ongezeko la 32% la idadi ya watoto waliolazwa katika vituo vya afya wakiwa na utapiamlo mkali wa ghafla pamoja na matatizo yanayohusiana nao, katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.
Takribani watoto milioni 1.9 wanatarajiwa kukabiliwa na utapiamlo nchini Somalia mwaka huu.
James Elder, msemaji wa UNICEF, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kupitia mkutano wa video kutoka Nairobi kwamba:
“Nchini Somalia leo, kupunguzwa misaada kunafunga milango ya huduma za afya, kusitisha huduma za lishe, na kufanya huduma za maji, elimu na ulinzi kuwa ngumu zaidi kufikiwa.”
Elder amesema hadi vituo 618 vya afya vinaweza kufungwa kote nchini endapo hali mbaya zaidi ya upungufu wa fedha itatokea.
Somalia inakabiliwa na ukame mkali ambao umeua mifugo, kuharibu mazao na kuangamiza vyanzo vya maisha vya watu. Mashirika ya misaada yanakadiria kuwa ukame uliwalazimisha takribani watu 500,000 kuyahama makazi yao kati ya Januari na Aprili, na kuongeza idadi ya Wasomali waliokwisha kuyahama makazi yao hadi takribani milioni 3.3.
Takribani theluthi moja ya wakazi milioni 19 wa Somalia wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Hata hivyo, fedha za kukabiliana na utapiamlo mkali katika baadhi ya maeneo ya Somalia zimepungua kwa zaidi ya asilimia 80 mwaka huu, kulingana na Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).