WHO: Mapigano yasitishwe DRC kwa angalau miezi sita ili kukomesha mripuko wa ebola
Wakati mripuko wa ugonjwa wa ebola unaendelea kuenea kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito wa kusitishwa mapigano kwa sababu za kibinadamu kwa muda wa angalau miezi sita, ili kuwezesha timu za afya kuwafikia watu walio katika hatari na kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo hatari.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kanda ya Afrika ya WHO, Dkt. Mohamed Yakub Janabi wakati wa ufunguzi wa kikao cha 76 cha WHO Kamati ya Kanda ya Afrika, kilichofanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, akibainisha kwamba, zana za kukabiliana na ebola zipo, lakini baadhi ya watu walioathirika bado hajawaweza kufikiwa na timu za afya.
Janabi amesema: “Changamoto iliyopo leo si ukosefu wa maarifa au zana” bali ni namna ya kuwafikia waathirika.
“Tunapoweza kuwafikia watu, tunazuia maambukizi. Tunaposhindwa kuwafikia, virusi vinaendelea kuenea,” ameeleza Dkt. Janabi.
Kwa mujibu wa shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa, kuzifikia jamii hivi sasa ndiyo kikwazo kikuu katika kukabiliana na mripuko wa ebola. Kwa sababu hiyo, WHO imezitaka pande zote hasimu kuhakikisha zinasitisha mapigano kwa sababu za kibinadamu kwa muda wa angalau miezi sita, ili timu za afya ziweze kuingilia kati “kwa usalama na bila vikwazo katika jamii zilizoathirika.”
Katika taarifa ya pamoja, Dkt. Janabi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, na Mkurugenzi Mtendaji wa Afrika wa kituo cha kudhibiti magonjwa CDC Dkt. Jean Kaseya, wametoa wito wa kufikiwa kila eneo lililoathirika, kulindwa kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele na ahadi kutafsiriwa kuwa hatua za vitendo.
“Juhudi hizi bado zinahitaji kuongezwa. Tunahitaji kuongeza mara mbili au tatu uwezo wa sasa wa mwitikio katika maeneo yake yote,” wameeleza maafisa hao wakuu wa afya.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni hadi Agosti 21, 2026, DRC ilikuwa imeripoti wagonjwa 5,514 waliothibitishwa na vifo 2,642 katika maeneo 57 ya afya.
Mripuko wa sasa wa ebola nchini humo unachukuliwa kuwa wa pili kwa ukubwa kuwahi kurekodiwa na unaoenea kwa kasi zaidi…/