Ndejembi apitishwa kwa 100% kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
-
Deogratius Ndejemba
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limempitisha Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kupata kura zote 324 zilizopigwa, sawa na asilimia 100.
Uamuzi huo umefanyika baada ya jina la Ndejembi kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupata ridhaa ya Wabunge, ambapo kura hizo zimeonyesha kuungwa mkono kwa asilia mia moja kwa uteuzi wake kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa Taifa.
Idadi ya kura za Hapana ilikuwa sifuri, huku kura halali zikiwa 324.
Kutokana na matokeo hayo, Spika wa Bunge ametangaza kuwa uteuzi wa Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeidhinishwa na Bunge kwa kura 324, sawa na asilimia 100.
Kuhusu kuteuliwa kwake katika nafasi ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, amesema ukubwa wa dhamana aliyopewa hautapimwa kwa umri au ujana wake, bali kwa utii kwa Rais wa Tanzania, uadilifu kwa Watanzania na utekelezaji wa majukumu atakayopewa.
Ndejembi amesema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa dhamana mbalimbali serikalini, ikiwemo kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Waziri wa Nishati, kabla ya kumteua kuwa Makamu wake wa Rais.
Amesema uteuzi huo ni ishara ya imani kubwa aliyooneshwa na Rais Samia, na ameahidi kutumia nafasi hiyo kwa unyenyekevu katika kumsaidia Rais kutekeleza majukumu yake na kuwa kiungo kwa Watanzania.
“Nafahamu ukubwa wa dhamana hii hautapimwa kwa ujana wangu peke yake. Dhamana yangu itapimwa kwa utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uadilifu kwa Watanzania na kazi yoyote nitakayotumwa na mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Ndejembi.
Deogratius Ndejemba anachukua nafasi iliyobakia wazi baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dakta Nchimbi kutangaza kujiuzulu siku chache zilizopita.
Baadaye Chama cha Mapinduzi (CCM) kilimfukuza uanachama Emmanuel Nchimbi, siku moja baada ya kujiuzulu wadhifa huo na kutangaza kustaafu siasa na utumishi wa umma, kwa sababu ya kile kilichotajwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili.