Sheikh Zakzaky: Vita dhidi ya Iran ni mwendelezo wa vita vilivyopiganwa dhidi ya Mtume Muhammad (SAW)
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141102-sheikh_zakzaky_vita_dhidi_ya_iran_ni_mwendelezo_wa_vita_vilivyopiganwa_dhidi_ya_mtume_muhammad_(saw)
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky, ameelezea vita vinavyoendelea, vilivyoanzishwa na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mhimili wa Muqawama kuwa ni mwendelezo wa vita vilivyowahi kupiganwa dhidi ya Mtume Muhammad (SAW) katika jaribio la kuzuia haki kutawala.
(last modified 2026-08-31T11:30:30+00:00 )
Aug 31, 2026 11:29 UTC
  • Sheikh Zakzaky: Vita dhidi ya Iran ni mwendelezo wa vita vilivyopiganwa dhidi ya Mtume Muhammad (SAW)
    Sheikh Zakzaky: Vita dhidi ya Iran ni mwendelezo wa vita vilivyopiganwa dhidi ya Mtume Muhammad (SAW)

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky, ameelezea vita vinavyoendelea, vilivyoanzishwa na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mhimili wa Muqawama kuwa ni mwendelezo wa vita vilivyowahi kupiganwa dhidi ya Mtume Muhammad (SAW) katika jaribio la kuzuia haki kutawala.

Sheikh Zakzaky amesema hayo mjini Abuja katika hotuba yake ya kufunga Kongamano la Wiki ya Umoja mwaka huu.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo mashuhuri wa Kiislamu nchini Nigeria, Mtume Muhammad (SAW) alikuja na ujumbe uliolenga kumpwekesha Mwenyezi Mungu (Tawhidi), kusimamisha uadilifu na kupinga dhulma.

Amesema kuwa nguvu zilizompinga Mtume zamani zilisukumwa na chuki dhidi ya haki na ujumbe wa Mwenyezi Mungu; na kwamba, hali kama hiyo ndiyo inayojidhihirisha katika mzozo wa sasa wa eneo la Asia Magharibi.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria amesisitiza kwamba Waislamu wanapaswa kuungana chini ya bendera moja ili kukabiliana na maadui zao. Akizungumza mifarakano na migawanyiko ndani ya jamii ya Kiislamu, Sheikh Zakzaky amewataka Waislamu wajifunze namna Iran inavyosisitiza umoja.

Alitoa mfano wa Tehran, akisema kwamba jiji hilo lina mkusanyiko mmoja mkuu wa swala ya Ijumaa, jambo alilolielezea kuwa ni ishara ya umoja na nguvu ya pamoja miongoni mwa Waislamu.

Akiashiria ukatili na unyama unaofanywa na maadui wa ubinadamu, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria amelaani mashinikizo ya kijeshi na kiuchumi yanayoendelea kufanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Aidha amezilaani Marekani na Israel kwa kuwalenga kwa makusudi wanafunzi wa shule katika mji wa Minab nchini Iran, akibainisha kuwa, shule hiyo ilishambuliwa mara tatu kwa lengo la kuwaua watoto.

Sheikh Zakzaky pia alisisitiza kuwa Iran sasa imeibuka na kuwa nguvu ya kimataifa, licha ya mashinikizo ya kijeshi yanayoikabili.