Rais wa Algeria aamuru kutekelezwa adhabu ya kifo kwa wale wanaochoma moto misitu kimakusudi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141112-rais_wa_algeria_aamuru_kutekelezwa_adhabu_ya_kifo_kwa_wale_wanaochoma_moto_misitu_kimakusudi
Rais wa Algeria aamuru kutekelezwa adhabu ya kifo kwa wale wanaochoma moto misitu kimakusudi
(last modified 2026-09-01T03:10:49+00:00 )
Sep 01, 2026 03:09 UTC
  • Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune
    Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune

Rais wa Algeria aamuru kutekelezwa adhabu ya kifo kwa wale wanaochoma moto misitu kimakusudi

Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, amemwagiza Waziri wa Sheria wa nchi hiyo kuandaa rasimu ya marekebisho ya Kanuni ya Adhabu, ambayo itajumuisha adhabu ya kifo kwa yeyote anayechoma moto misitu kwa makusudi. Agizo hili limetolewa kufuatia wimbi la moto lililokumba majimbo kadhaa ya mashariki na kati mwa Algeria ambalo limesababisha vifo vya watu 12.

Uamuzi huo umechukuliwa katika mkutano ulioongozwa na Tebboune katika Ikulu ya Rais mjini Algiers ukihudhuriwa na maafisa wakuu wa kiraia na kijeshi, na umejadili hatua za kushughulikia athari za moto wa hivi karibuni.

Rais wa Algeria amemwagiza Waziri wa Sheria, Hafez Al-Akhtam Lotfi, kurekebisha kanuni ya adhabu kabla ya Septemba 15 ili kujumuisha adhabu ya kifo kwa wale waliohusika katika kuchoma moto misitu kwa makusudi.

Televisheni ya serikali imeeleza kwamba Rais wa Algeria ameamuru kwamba adhabu kwa wahusika wa uhalifu wa moto wa misitu ziongezwe ili kujumuisha adhabu ya kifo, na itekelezwe baada ya kutumia njia zote za kukata rufaa zinazodhaminiwa na sheria.

Adhabu kubwa zaidi zinazotumika kwa uhalifu kama huo kwa sasa ni kifungo cha miaka 30 au kifungo cha maisha jela katika baadhi ya matukio.

Tebboune amesisitiza haja ya kuwasilishwa rasimu ya marekebisho hayo ya sheria serikalini wiki hii kabla ya kuipeleka kwenye Bunge la Taifa, akisisitiza kwamba "yeyote anayeamini kwamba sheria haitatumika anapaswa kujua kwamba jamii na mkono wa uadilifu vitatenda haki."

Mapema Jumamosi, Rais wa Algeria alisema kwamba kuna uwezekano kuwa kile alichokiita "mikono ya wahalifu" ndiyo sababu ya moto mkubwa ulioteketeza misitu katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo, akisisitiza kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini sababu za matukio hayo.