Watu 5 waliopona Ebola waruhusiwa kurejea nyumbani Kongo huku idadi ya maambukizi ikipindukia 6,000
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141122-watu_5_waliopona_ebola_waruhusiwa_kurejea_nyumbani_kongo_huku_idadi_ya_maambukizi_ikipindukia_6_000
Watu watano waliopona ugonjwa wa Ebola jana waliruhusiwa kutoka katika kituo cha matibabu huko Béni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2026-09-01T14:17:17+00:00 )
Sep 01, 2026 14:15 UTC
  • Watu 5 waruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupona Ebola Kongo
    Watu 5 waruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupona Ebola Kongo

Watu watano waliopona ugonjwa wa Ebola jana waliruhusiwa kutoka katika kituo cha matibabu huko Béni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Watu hao waliopona Ebola, akiwemo mfanyakazi wa sekta ya afya, walikuwa wamelazwa katika kituo cha matibabu ya Ebola cha shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) na katika kituo cha matibabu ya Ebola cha Hospitali ya Béni.

Baada ya kupokea cheti kinachothibitisha kuwa wamepona, manusura hao walitoa shukrani kwa timu za matibabu zilizowahudumia na kuwahimiza wananchi wenzao kutafuta matibabu pale watakapobainika kuwa na maambukizi.

Wafanyakazi wa afya na maafisa wanaoongoza juhudi za kukabiliana na Ebola wamesherehekea kuruhusiwa watu hao watano na kurejea nyumbani, huku kiongozi wa muungano wa kukabiliana na Ebola akisema kuwa jana ilikuwa "siku muhimu sana" na "chanzo cha fakhari kwa" timu yake.

Hii ni katika hali ambayo idadi ya wagonjwa wa Ebola inaendelea kuongezeka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na manusura hao wameruhisiwa kutoka hospitalini huku mamlaka za husika za afya zikitangaza kuwa wagonjwa wa Ebola sasa wamepindukia 6,000.

Mamlaka hizo pia zimearifu kuwa mlipuko huo ambao maambukizi yake yalikuwa na kasi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umesababisha vifo vya 2,911.

Zaidi ya watu 1,360 wamepona Ebola katika hatua ambayo mamlaka za afya za Kongo zimeitaja kuwa ya "kutia moyo."