Ripoti: Gaddafi wa Libya alimuua Imamu Musa Sadr kwa kumpiga risasi mbili kifuani
Aliyekuwa dikteta wa Libya, Muammar Gaddafi, anadaiwa kumpiga risasi mbili kifuani mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu kutoka Lebanon, Allamah Imamu Musa Sadr, baada ya Imamu kukosoa vikali kile kilichoitwa “Kitabu cha Kijani” (The Green Book) na kukitaja kuwa cha kipuuzi na kisicho na mashiko, huku akimueleza mwandishi wake kama mtu mwenye hitilafu ya kiakili. Ufichuzi huu umetolewa na mwanahistoria, mtafiti na mwanahabari maarufu wa Iraq, Dkt. Hamid Abdullah.
Dkt. Abdullah alitoa masimulizi hayo ya kihistoria kuhusu kadhia ya kutoweka kwa Imamu Sadr na wenzake wawili, Sheikh Mohammad Yaacoub na mwanahabari Abbas Badreddine, kupitia kipindi chake kwenye jukwaa la YouTube.
Amesisitiza kuwa simulizi hii inajikita kimsingi kwenye nyaraka za kiintelijensia zilizopokelewa na idara ya ujasusi ya Iraq wakati huo kutoka kwa afisa wa usalama wa Libya aliyekuwa na mafungamano ya moja kwa moja na utawala wa Gaddafi.
Abdullah alieleza zaidi kwamba nyaraka hizo muhimu zinazohusiana na jinai ya kutoweshwa kwa Imamu bado zipo nchini Iraq hadi hivi sasa.
Kwa mujibu wa Dkt. Abdullah, mnyororo wa taarifa hizi ulianzia kwa aliyekuwa Kanali wa kijeshi wa Libya na mwanachama wa chama cha Ba’ath, Salim al-Hajani, ambaye alikimbilia Baghdad kuomba hifadhi ya kisiasa. Kanali huyo aliifahamisha idara ya ujasusi ya Iraq kuhusu kuwepo kwa afisa wa ngazi ya juu katika idara ya usalama wa nje ya Libya, Mohammad Ahmad al-Adl, aliyekuwa na siri nzito na nyeti kuhusu utawala wa kibabe wa Gaddafi.
Kufuatia hatua hiyo, kikao cha siri kilipangwa kati ya Al-Adl na maafisa wa Iraq katika ubalozi wa Iraq mjini Tunis. Ripoti hiyo inabainisha kuwa Al-Adl baadaye aligeuka kuwa mtoa taarifa mkuu wa ujasusi wa Iraq, akiwapa taarifa mbalimbali za ndani, zikiwemo nyaraka mahususi kuhusu faili la Imamu Sadr.
Abdullah anabainisha kuwa Al-Adl alipata maelezo haya ya kina kutoka kwa mmoja wa walinzi wa kike wa Gaddafi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, chanzo cha mzozo huo kilianza wakati utawala wa Gaddafi ulipokuwa ukitoa misaada ya kifedha kwa makundi mbalimbali nchini Lebanon wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwemo Harakati ya Amal iliyoongozwa na Imamu Sadr. Wakati huo huo, Gaddafi alikuwa akijaribu kusambaza na kupigia debe “Kitabu chake cha Kijani” nje ya mipaka ya Libya. Nakala za kitabu hicho zilifikishwa Lebanon, na Imamu Sadr alipata fursa ya kukisoma na kukitathmini.
Mnamo tarehe 25 Agosti 1978, Imam Musa Sadr aliwasili nchini Libya kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa mamlaka za Libya. Kwa mujibu wa masimulizi yaliyotolewa na Dkt. Abdullah, Gaddafi alitaka kufanya mazungumzo ya faragha na Imamu Sadr mnamo Agosti 31 katika ngome yake ya kijeshi ya Bab al-Aziziya, akisisitiza kuwa wenzake wawili walioandamana naye wasihudhurie kikao hicho.
Katika kikao cha ana kwa ana, Gaddafi alimkabili mgeni wake huyo mtukufu kuhusu ripoti alizopokea, akimuuliza iwapo ni kweli alikikejeli kitabu hicho na kukiita chapisho la kipuuzi. Imamu Sadr hakurudi nyuma wala hakutumia lugha ya kujipendekeza au unafiki; badala yake, “alieleza msimamo wake wa haki kwa ujasiri usio na woga, akibainisha wazi kuwa kitabu hicho kilikuwa tupu na hakikubeba nadharia wala fikra yoyote yenye thamani ya kielimu au ya kimaadili.”
Baada ya kutekeleza jinai hiyo ya mauaji, Gaddafi na genge lake la karibu walikabiliwa na mtihani mzito wa jinsi ya kupoteza miili hiyo na kufuta kabisa athari za uhalifu wao.
Kwa mujibu wa maelezo ya Abdullah, afisa mmoja aliyejulikana kama Ahrari alipewa amri madhubuti ya kuisafirisha miili ya mashahidi hao watatu na kuizika kwa siri katika eneo la Bir al-Ghanam, lililoko magharibi mwa Libya.