Guinea-Bissau yapiga kura ya 'ndiyo' katika kura ya maoni ya katiba mpya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141150-guinea_bissau_yapiga_kura_ya_'ndiyo'_katika_kura_ya_maoni_ya_katiba_mpya
Wapigakura nchini Guinea-Bissau wameidhinisha mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maoni ambayo itampa rais mamlaka zaidi.
(last modified 2026-09-02T12:52:56+00:00 )
Sep 02, 2026 12:49 UTC
  • Guinea- Bissau yaunga mkono kura ya maoni
    Guinea- Bissau yaunga mkono kura ya maoni

Wapigakura nchini Guinea-Bissau wameidhinisha mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maoni ambayo itampa rais mamlaka zaidi.

Haya yamebainishwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu unaolenga kurejesha utawala wa kiraia nchini humo.

Kura ya maoni ya Jumapili iliyopita nchini Guinea-Bissau ilifanyika chini ya miezi 10 baada ya mapinduzi ambapo jeshi lilichukua madaraka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, na ikiwa imesalia miezi michache tu kabla ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika tarehe 6 Desemba.

Guinea-Bissau ni mfano wa hivi karibuni wa hatua zilizochukuliwa katika miaka ya karibuni na viongozi wa mataifa kadhaa ya Afrika wanaotaka kurekebisha au kubadilisha kikamilifu katiba ya nchi zao ili kuongeza muda wa uongozi, kuondoa vikwazo vya umri au kupanua mamlaka ya serikali wakifuata nyayo za Zimbabwe, Guinea, Togo, Uganda na Chad.

Kwa mujiibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo kambi ya "ndiyo" imeibuka mshindi kwa asilimia 70 ya kura.

Baraza la Uongozi wa Kijeshi la Guinea-Bissau limesema kuwa mabadiliko hayo yataimarisha taasisi za nchi kabla ya uchaguzi wa rais uliopangwa kurejesha madaraka kwa raia baadaye mwaka huu.

Hata hivyo, hali ya kisiasa ni ya taharuki katika taifa hilo la pwani lenye historia ya mapinduzi ambapo wapinzani walikuwa wamewahimiza wananchi kutoshiriki katika kura hiyo ya maoni.

Kwa upande wake Jenerali Horta N'Tam kiongozi wa Baraza la Kijeshi na rais wa serikali ya mpito wa Guinea-Bissau aliwatolea wito vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika zoezi hilo la kura ya maoni iliyofanyika Jumapili iliyopita.